GENEVA:Fedha zaidi na haraka zahizitajika kunusuru maisha ya watu Pakistan
26 Oktoba 2005Mratibu mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Rashid Khalikov,amesema watu wengi zaidi huenda wakafa kutokana na athari zinazowanyemelea,baada ya tetemeko kubwa la ardhi kupiga nchini Pakistan,kuliko ilivyotokea wakati wa tetemeko lenyewe,iwapo mataifa wafadhili yanayokutana mjini Geneva hayatatoka na azimio la kutoa fedha zaidi haraka.
Watu waliokufa kutokana na tetemeko la ardhi la tarehe 8 mwezi huu wanaojulikana hadi sasa ni 54,000,lakini hivi sasa muda unawapita wafanyakazi wanaotoa misaada kuweza kuwafikia maelfu ya watu kabla msimu wa baridi kali haujaanza.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema kiasi cha watu milioni tatu wanahitaji misaada ya haraka.
Hadi sasa nchi wahisani zimetoa kiasi kidogo sana cha fedha kinachohitajiwa ili kuwalinda watu walionusurika na tetemeko la Oktoba nane na pia kuweza kuzuia vifo zaidi.