Gaza yakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi
4 Agosti 2025Mzozo wa maji safi ambao haujawahi kushuhudiwa unaendelea kote Gaza, na hivyo kuzidisha masaibu kwa wakaazi wa eneo hilo la Palestina. Gaza ilikuwa tayari inakabiliwa na tatizo la maji kabla ya kuanza kwa vita hivi kati ya Israel na Hamas ambavyo vimeharibu zaidi ya asilimia 80 ya miundombinu ya maji katika Ukanda huo.
Wakati mwingine, malori ya maji huwafikia wakazi na mashirika yasiyo ya kiserikali huweka mabomba kwenye kambi za wachache waliobahatika, lakini juhudi zote hizo haitoshi.
Israel iliunganisha baadhi ya mitambo ya maji kaskazini mwa Gaza na kampuni ya maji ya Israel ya Mekorot, baada ya kukata maji mwanzoni mwa vita hivyo, lakini wakaazi wa eneo hilo wanasema hadi sasa maji bado hayatoki.
Msemaji wa Jiji la Gaza Assem al-Nabih ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mitambo ya sehemu ya jiji hilo iliyounganishwa na mtandao wa shirika la maji la Israel Mekorot haijafanya kazi kwa karibu wiki mbili sasa.
Raia wa Gaza hawawezi kuvifikia visima
Visima ambavyo vilikuwa vikikidhi mahitaji ya maji kabla ya vita pia vimeharibiwa, huku vingine vikichafuliwa na maji taka. Ni vigumu kuvifikia visima vingi vya Gaza kwa sababu vinapatikana kwenye maeneo ya mapigano, karibu na vituo vya jeshi la Israel au katika maeneo ambapo raia wameamriwa kuondoka.
Nisreen Al Tamimi, ni mkuu wa Mamlaka ya Ubora wa Mazingira huko Gaza: " Vita hivi vimesababisha madhara makubwa kwa binaadamu na mazingira. Vimeathiri mfumo mzima wa ikolojia pamoja na uchafuzi wa hewa, maji, mashamba, ukataji miti na mfumo wa kusafisha maji taka na kuporomoka kwa mfumo wa afya. Athari za vita hivi zimeenea katika mfumo mzima wa ikolojia."
Miito ya kutolewa misaada zaidi Gaza
Serikali ya Australia imeahidi leo kutoa misaada zaidi ya kibinadamu kwa wanawake na watoto, siku moja baada watu wapatao 90,000 kuandamana katika mji mkuu Sydney wakipinga yanayoendelea katika Ukanda huo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong ametangaza nyongeza ya dola milioni 13 katika kifurushi cha msaada wa kibinadamu kwa Gaza na hivyo kupelekea ahadi ya Australia kufikia dola milioni 130 za kuwasaidia raia wa Gaza na Lebanon.
Israel imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji kimataifa kutokana na hatua zake zinazopelekea kuenea kwa njaa, lakini imekuwa ikikanusha hilo na kusema kila wakati imekuwa ikiruhusu usambazaji wa misaada katika Ukanda huo wanakoishi Wapalestina zaidi ya milioni mbili.
// DPA, Reuters, AFP