Gaza: Moshi mzito wapaa karibu na hospitali ya Nasser
1 Agosti 2025Mlipuko uliofuatiwa na moshi mzito karibu na mji wa Khan Younis, katika Ukanda wa Gaza umetokea mapema Ijumaa wakati jeshi la Israel linapoendelea na mashambulizi yake katika eneo hilo.
Daktari wa watoto Thomas Adamkiewicz, Mmarekani anayefanya kazi kati hospitali ya Nasser amesema anatamani Mjumbe maalum wa Rais Trump afike kwenye hospitali hiyo.
Daktari Adamkiewicz, amesema:- "Wapo watoto wanaokufa kwa njaa hapa. Nimewaona kwa macho yangu. Bwana Witkoff atakuwa sehemu ambayo si mbali na hapa. Kama inawezekana ningetaka nimwalike aje ili ajionee mwenyewe kinachoendelea hapa."
Mjumbe maalum wa Rais wa Marekani Donald Trump, bwana Steve Witkoff, aliwasili Alhamisi nchini Israel kwa ajili ya kufanya majadiliano juu ya hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Wakati huo huo idadi ya vifo vya Wapalestina waliokuwa wakisubiri chakula na misaada mingine inaendelea kuongezeka. Takriban Wapalestina 91 wameuawa na wengine zaidi ya 600 wamejeruhiwa walipokuwa wanasubiria kupata msaada katika muda wa saa 24 zilizopita, hayo ni kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.
Ikulu ya Marekani imesema, Mjumbe maalum wa Rais Donald Trum, Steve Witkoff na Balozi wa Marekani nchini Israel, Mike Huckabee siku ya Ijumaa watakagua usambazaji wa chakula huko Gaza.
Witkoff atakutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kabla ya ziara hiyo ya kukagua usambazaji wa misaada huko Gaza, huku jamii ya kimataifa ikizidisha shinikizo la kusitishwa kwa mapigano.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul, anaendelea na ziara yake ya siku mbili nchini Israel na katika eneo la Palestina na hii leo atakuwa katika Ukingo wa Magharibi ambako atakutana na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas katika mji wa Ramallah.
Mazungumzo yao yanatarajiwa kuangazia ghasia zinazofanywa na walowezi wa Kiyahudi dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na juu ya mapendekezo ya Israel kuhusu uwezekano wa kulinyakua eneo hilo.
Bunge la Israel, wiki iliyopita lilipitisha azimio linalounga mkono Israel kulijumisha eneo hilo katika maeneo yake. Hata hivyo hatua hiyo ambayo haifungamani na sheria za Israel imekosolewa kimataifa ikiwemo Ujerumani ambayo ni mshirika mkuu wa Israel.
Ujerumani pia inatazamiwa kutoa fedha nyingine za msaada zipatazo dola milioni 5.7 kwa raia wa Ukanda wa Gaza. Waziri wa Mambo ya Nje Johann Wadephul, amesema pesa hizo zitakwenda kwenye mashirika ya Mpango wa Chakula ya Umoja wa Mataifa.
Waziri Wadephul ametoa wito kwa serikali ya Israel kuanza haraka ushirikiano na Umoja wa Mataifa na mashirika yake ili kuboresha usambazaji wa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza unaokabiliwa na vita.
Wakati huo huo Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, siku ya Ijumaa limevilaumu vikosi vya Israel kwa kuwaua raia wa Palestina wanaotafuta chakula, pamoja na kutumia njaa kama silaha ya vita.
Lawama hizo zimeelekezwa kwa vikosi vinavyofanya kazi katika maeneo vilivyopo vituo vya kutolea misaada. Vituo hivyo vinaendeshwa na Taasisi ya misaada ya GHF, linaloungwa mkono na Marekani na Israel katika Ukanda wa Gaza.
Vyanzo: DPA/AFP