Gavana wa kijeshi wa Kivu Kaskazini apigwa risasi
24 Januari 2025Shirika la habari la Ufaransa AFP limeripoti kwamba gavana wa jimbo la Kivu Kaskazini, Jenerali Peter Chirimwami amefariki Ijumaa kufuatia majeraha baada ya kupigwa risasi hapo jana kwenye uwanja wa mapambano. Hata hivyo serikali bado haijatangaza rasmi kifo chake.
Rais wa Kongo Felix Tshisekedi anaongoza mkutano wa baraza la ulinzi mjini Kinshasa, kufuatia ule alioitisha jana usiku.
Msemaji wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa Mathew Saltmarsh amesema huko Geneva kwamba wakimbizi wa ndani zaidi ya laki nne wamekimbia makwao mnamo kipindi cha wiki tatu huko Kivu ya Kaskazini na Kivu Kusini.
"Mashambulizi kutokana na makabiliano haya yalizilazimisha familia nyingi kuyakimbia makambi yaliyo nje ya Goma wakijaribu kutafuta maeneo salama ndani ya mji. Wafanyakazi wetu, wa shirika la UNHCR wamebakia huko Goma kuwasaidia wale waliokimbia kwa jinsi wanavyoweza. Lakini kama unavyoelewa, kuyafikia maeneo hayo kwa sasa ni ngumu sana.", alisema Saltamarsh.
Wanajeshi wa Monusco na SADC kushirikiana na jeshi la Kongo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alielezea masikitiko yake kufuatia kuendelea kwa mapigano. Antonio Guterres amesema mashambulizi haya yana madhara makubwa kwa raia na kuongeza hatari ya kuzuka kwa vita vya kikanda.
Mapigano yalizuka mapema Ijumaa kilomita 20 tu kutoka mji wa Goma. Duru za kijeshi zimesema kwamba mapambano makali yanaendelea kwenye viji vya Kibumba na Kanyamahoro.
Duru hizo zimesema kuwa waasi wa M23 wanaendelea kushikilia mji wa Sake kusini mwa mji wa Goma.
Helikopta za jeshi la Kongo pia zilionekana ziki washambulia waasi wa M23 kwenye mji huo wa Sake.
Kamanda wa vikosi vya umoja wa mataifa nchini Kongo, MONUSCO, Jenerali Khar Diouf, alisema Ijumaa kwamba wanajeshi wake na wale wa nchi za jumuiya ya kiuchumi ya kusini mwa Afrika SADC wanashirikiana na jeshi la Kongo ili kulinda raia na kuulinda mji wa Goma pamoja na mji wa Sake.
Baadhi ya wakaazi wa Goma wamesema kwamba vifaru vya jeshi la Monusco vilionekana vikielekea magharibi mwa mji huo ambako pia mapigano yaliripotiwa Ijumaa asubuhi.