Gachagua kuzindua chama chake kwenye ukumbi binafsi
4 Juni 2025Rigathi Gachagua alijiuzulu kutoka chama tawala cha UDA na kuunda chama chake kwa jina la DCP ambacho kilipangiwa kuzinduliwa rasmi hii leo katika uwanja wa Kasarani.
Hata hivyo, hatua ya Shirika la Usimamizi wa Viwanja vya Michezo nchini, Sports Kenya, kubatilisha uamuzi wake wa awali wa kuwakodisha uwanja wa michezo wa Kasarani umewaacha viongozi wa chama hicho kipya kwenye njia panda.
Cleophas Malala, ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha DCP, anailamu serikali kwa masaibu yao.
"Tulitakiwa kuzindua chama chetu huko Kasarani tarehe 3 Juni, hata hivyo serikali iliamua kutunyima uwanja huo", alisema Malala.
Chama hicho kinadai kuwa kiliiandikia barua Sports Kenya na kuomba kutengewa uwanja huo kwa ajili ya hafla yao na wakaarifiwa kuwa wangelipata kibali, lakini baadaye shirika hilo lilibadilisha msimamo na kuwaarifu kuwa uwanja huo utakuwa ukitumika na wanaspoti.
"Chama cha UDA hakimjali mwananchi"
Viongozi wa DCP wanaikosoa serikali kwa kile walichokiita ukandamizaji wa upinzani, na wanayaona matukio haya kama njama ya kuwanyamazisha. Aliyekuwa mbunge wa Laikipia, Kate Waruguru, ambaye sasa ni mmoja wa viongozi wa chama cha DCP amekikosoa vikali chama tawala.
"Chama cha UDA hakimjali mwananchi ndiyo maana tunasema sisi ndio chama kinachomsikiliza mwananchi wa kawaida."
Wakosoaji wanasema, Naibu Rais wa zamani Gachagua amekuwa mzigo kwa taifa, huku siasa zake zikijikita katika uchochezi wa kikabila, kisasi cha kibinafsi, na mashambulizi ya kimakusudi dhidi ya utangamano wa kitaifa.
Wanadai kile wanachokiita matusi yake ya hivi majuzi hadharani kwa wabunge wa Mlima Kenya ambapo aliwatusi kwa kuunga mkono serikali, sio ushujaa wa kisiasa tu bali ni jaribio la kuzivunja jamii na kudhoofisha uongozi wa kidemokrasia.
Baadhi ya wabunge wanaounga mkono serikali wameikosoa mienendo yake wanayoyaita ya uchochezi.
Viongozi wa DCP, hata hivyo, wanasisitiza kuwa harakati zao za kukizindua rasmi chama chao bado zinaendelea na wamewaarifu wanachama wao kwamba wanatafuta sehemu mbadala na kwamba watazikindua chama hicho ndani ya mwezi huu.