Gachagua arejea kwa kishindo akitokea ziarani Marekani
21 Agosti 2025Mbwembwe vifijo na nderemo vilirindima sehemu kubwa ya Alhamisi katika uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta punde wafuasi wa Gachagua walipokuwa wakimsubiri kiongozi huyo. Naibu wa Rais huyo wa zamani amekuwa nchini Marekani kwa kipindi cha wiki sita zilizopita.
Akiwa nchini Marekani, Gachagua aliitumia ziara hiyo kuikosoa vikali serikali ya Kenya Kwanza aliyoitumikia wakati mmoja. Gachagua ambaye alionekana kuwa na furaha tele alikuwa amevalia kofia, suruali na shati ya jeans za rangi ya samawati huku nyimbo za kumpinga Ruto zikisikika angani pembezoni mwa Barabara ya Mombasa.
Kuwasili kwake kulizua shamrashamra, huku umati wa watu ukipanga mstari kando ya barabara kutoka uwanja wa Jomo Kenyatta kuelekea katikati ya jiji la Nairobi, wakibeba mabango na kuimba kaulimbiu za kukiunga mkono chama chake cha Democracy for Citizens Party, DCP. Viongozi kutoka Mlima Kenya anakotokea Gachagua walikuwa mstari wa mbele kumpokea.
Seneta wa Murang'a Joe Nyotu aalikuwa miongoni mwao, ''Kufika hapa hatajaona vurugu zozote kutoka kwa polisi, ni vizuri ifahamike kuwa mara nyingi wanaoleta vurugu ni polisi. Tumekuja kwa amani polisi wasipotuvuruga siku hii itaisha kwa amani.'' alisema.
Polisi yaimarisha ulinzi katika uwanja wa ndege
Idara ya Polisi ya Taifa iliimarisha ulinzi mkali katika uwanja wa ndege na maeneo ya jirani, kwa kupelekwa magari ya maji ya kuwasha na kuzima ghasia, vikosi vya kupambana na fujo, pamoja na helikopta kwa ajili ya doria za angani. Maafisa usalama walidumisha utulivu wakati mamia ya wafuasi walipojaribu kuingia ndani ya uwanja wa ndege.
Ripoti zinaashiria alikatiza kuwa Gachagua ziara yake Marekani na kurejea nchini kuongoza kampeni za chama chake cha DCP katika chaguzi ndogo mbalimbali zilizopangwa kufanyika Novemba 27, ikiwa ni pamoja na uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malava, magharibi mwa Kenya. Mwangi Muraya ni mfuasi sugu wa Gachagua.
Mwangi Muraya ni miongoni mwa wafuasi kindakindaki wa Gachagua amesema "Tumekuja hapa ili tuweze kumlaki kiongozi wetu. Tutaendelea na kempeni na shughuli za kuhakikisha kuwa tunaiondoa Kenya Kwanza kwenye uongozi, hii wanashinda hapa wakituambia KBB ni kuiba bila breki.”
Gachagua anatarajiwa kuongoza maandamano kuelekea viwanja vya Kamukunji kwa ajili ya mkutano wa hadhara, hatua ambayo serikali imeahidi kuifuatilia kwa makini ili kuzuia machafuko. Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, amesema kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa endapo kutatokea vurugu na usumbufu.