Njia iliyotumika enzi za biashara ya utumwa Afrika Mashariki
15 Agosti 2025Ujio wa Sultan Seyyid Said kutoka Muscat Oman katika kisiwa cha Zanzibar mwaka 1840 unaelezwa kuwa ulichochea kukua kwa biashara ya utumwa kutokana na ongezeko la uhitaji wa nguvu kazi ya mwanadamu katika kilimo cha karafuu ambacho aliakianzisha kisiwani humo. Kukua kwa biashara ya utumwa kunaelezwa pia kulichochewa na mataifa ya Ulaya na Marekani yaliyokuwa na mashamba yake katika nchi ya Mauritius, Reunion na mataifa mengine ya Amerika Kusini.
Uhitaji huo ulisababisha wafanyabiashara hususan Waarabu na Waswahili wachache ambao walikuwa na mchanganyiko na Waarabu akiwemo Hamad Bin Muhammed bin Mujerbi almaarufu kwa jina la Tippu Tip kuanza safari za kuelekea Bara kwa ajili ya kuwanunua binadamu na kisha kuwafanya watumwa.
Simulizi za wataalamu wa Historia na zile za Watemi hususan wale waliopitiwa na biashara hiyo katika njia ya kati ya utumwa iliyoanzia Bagamoyo hadi Ujiji Kigoma, zinasema kuwa wafanyabiashara hao waliwanunua watumwa kutoka kwa Watemi ambao nao walikuwa wamewakamata mateka watu hao baada ya kuvamia na kuushinda Ufalme mwingine.
Wanazuoni wataka ukimya kuhusu biashara ya watumwa uvunjwe
Dokta Salvatory Nyanto ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa masuala ya historia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania anasema ni wakati wa kuvunja ukimya kuhusiana na biashara hiyo ya utumwa kwani ni sehemu muhimu ya historia ya nchi.
''Suala zima la utumwa ni suala la aibu na watu wengi wamekuwa wanaona aibu kujitambulisha kwamba aidha wao ni vizalia au walikuwa sehemu ya historia hii na ndio maana kutokana na aibu hii iliyojengeka katika jamii imekuwa ni vigumu zaidi kuzungumza masuala haya,'' alifafanua Dokta Nyanto.
Kulingana na Mhadhiri Mwandamizi wa masuala ya historia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia watu wamekuwa wanaogopa kujitambulisha kuwa sehemu ya historia hiyo, lakini anadhani ni suala ambalo wao kama watafiti wana jukumu la kuielimisha na kuieleza jamii kwamba hii ni sehemu ya historia ya nchi yao, ni sehemu ya historia ya Tanzania na huu ni urathi wa historia yao na maisha yao.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Hifadhi za Taifa, TANAPA kwa kushirikiana na Dokta Nyanto ulibaini maeneo 14 yenye ushahidi unaoonekana wa kupitiwa na misafara ya wapagazi na watumwa katika njia ya kati iliyotumika katika biashara hiyo. Mhadhiri huyo anasema ushahidi katika maeneo hayo unajumuisha njia yenyewe, makanisa ya kale ambayo yalitumika kukomesha biashara hiyo, alama zilizowekwa na wamisionari pamoja na masalia ya vitu vilivyokuwa vinatumika nyakati hizo.
Kituo cha kwanza kwa upande wa Kigoma ilikuwa ni bandari ya Bangu iliyopo katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika, ambayo kwa sasa ipo karibu kabisa na bandari ya Kigoma. Watumwa waliokuwa wametoka katika ukanda wa Kongo hapo ndio ilikuwa bandari yao ya kwanza kushushwa na kisha walipelekwa katika soko la Ujiji.
Wanazuoni wanasema hivyo safari ilianzia soko la Ujiji na ushahidi uliopo kwenye eneo lile kuna nyumba iliyokuwa ya Tippu Tip, aliyekuwa mfanyabiashara maarufu. Aidha, kuna miembe ambayo imebaki kama ushahidi kwamba hiyo ndio ilikuwa njia ambayo misafara ya wapagazi pamoja na watumwa ilipita ikielekea Pwani.
Wamisionari waliwasili Afrika Mashariki kupitia vyama vya kimisionari
Uhitaji wa nguvu kazi za binadamu katika viwanda ulianza kupungua baada ya kuanza kwa mapinduzi ya viwanda nchini Uingereza mwaka 1760 hali iliyochochea vuguvugu la kukomeshwa kwa biashara ya utumwa ili kutoa fursa kwao waanze kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda hivyo vya Ulaya katika maeneo hayo.
Wamisionari hususan wa kanisa la Anglikana walianza kuwasili katika eneo la Afrika Mashariki kupitia vyama vyao vya kimisionari kikiwemo cha Church Mission Society, CMS, na Universities Mission for Central Africa. Miongoni mwa wamisionari waliowasili katika kipindi hicho alikuwa Dokta David Livingstone ambaye alishiriki katika kukomesha biashara ya utumwa katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki na Kati.
Mmisionari mwingine aliyehusika katika kukomesha biashara hiyo alikuwa Edward Steere ambaye ndiye aliyelinunua eneo la Mkunazini, Zanzibar lililokuwa soko kuu la watumwa na kujenga kanisa la kwanza la Anglikana Tanzania mwaka 1873. Ujenzi wa kanisa hilo ukachochea makanisa mengine likiwemo lile la Mpwapwa, Dodoma lililojengwa mwaka 1876, nia ikiwa kuwakomboa watumwa.
Dokta George Lawi, Mchungaji na Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Tanzania anasema ni ngumu kuitenganisha historia ya kanisa hilo na biashara ya utumwa. ''Kanisa limejitahidi kuhifadhi historia ya utumwa, kwanza kupitia kwenye vitabu mbalimbali ambavyo vimechapishwa kwa muktadha wa kanisa. Jambo la pili ambalo limefanyika kama sehemu ya kutunza pia ni pamoja na kuhifadhi yale maeneo muhimu yanayobeba historia na kumbukumbu kubwa ya biashara ya utumwa,'' alibainisha Mchungaji Lawi.
Kwa mujibu wa mchungaji huyo, kanisa lao kuu pale Mkunazini eneo ambalo kanisa limejengwa, ndilo lilikuwa soko la watumwa, na kwamba ukiingia ndani ya kanisa utabaini wamechora alama nyekundu ambapo palikuwa sehemu ya watumwa kuchapwa. Mtumwa alikuwa akitolewa kwenye vyumba wanavyohifadhiwa anapelekwa eneo hilo anafungwa na kupigwa. Aidha, pembeni ya sehemu hiyo, kuna meza ambayo karani anakaa kupokea fedha baada ya bei ya mtumwa fulani kufikwa.
Serikali ya Tanzania imeanza kutazama historia hii ya utumwa kuwa fursa zaidi katika utalii wa kihistoria unaoweza kuwavuta zaidi watalii. Kama ilivyo kwenye baadhi ya maeneo mengine hususan kwa Zanzibar yameashaanza kuingiza fedha. Mathalani watalii kati ya 200 hadi 300 wanaingia kila siku katika kanisa la Anglikana lililopo Mkunazini.
TANAPA: Maeneo yaliyopitiwa na biashara ya utumwa kutumika kwa utalii
Nengai Nairouwa, Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi Malikale wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA, anasema maeneo mengine yaliyopitiwa na biashara ya utumwa yanaweza kutumika kama kivutio cha utalii. ''Maeneo haya yana thamani kubwa sana katika historia ya nchi, lakini ni maeneo ambayo yapo wazi yanathibitisha uwepo wa biashara ya utumwa na pembe za ndovu,'' alisema Nairouwa.
Nairouwa, anasema la kwanza la msingi ni kuyahifadhi ili yatumike katika utalii, lakini pia wanaoyasimamia maeneo hayo kwa sababu maeneo mengine yapo chini ya vijiji na halmashauri. Kwa hiyo wale wanaohusika na utalii wanatakiwa kuweka mpango kazi wa kuyasimamia maeneo hayo ili yaweze kutumika kiutalii na kuongeza Pato la Ndani la Taifa.
Sekta ya utalii Tanzania imekuwa ikichangia asilimia 17 katika Pato la Taifa. Serikali pamoja na wadau wa utalii wamekuwa wakitafuta mbinu za kuikuza zaidi sekta hiyo ambapo kwa sasa inaelezwa kuwa nguvu zinaelekezwa katika utalii wa kihistoria unaoyajumuisha maeneo yaliyopitiwa na biashara dhalimu ya utumwa.
Makala hii imeandaliwa na Anuary Mkama