FUJO VIWANJANI KABLA KOMBE LA DUNIA UJERUMANI
31 Machi 2005UJERUMANI IMEAPA KUIMARISHA USALAMA WAKATI WA KOMBE LIJALO LA DUNIA 2006
JAPAN-MABINGWA WA ASIA WAELEZEA WASI WASI WA KUCHEZA DIMBA KOREA YA KASKAZINI BAADA YA MKASA ULIOIKUMBA IRAN
RAIS WA (IOC) HALMASHAURI KUU YA OLIMPIK ULIMWENGUNI AKANUSHA KINYAN’GANYIRO CHA KUANDAA OLIMPIK 2012 NI CHA MIJI 3 NA
MICHAEL SCHUMACHER AMEJIWINDA KUTAMBA TENA KATIKA MBIO ZA KESHO ZA MAGARI HUKO MANAMA,BAHREIN.hayo na mengineo, ndio niliowaandalia jioni hii:
Kati ya wiki hii kinyan’ganyiro cha kuania tiketi za Kombe lijalo la dunia nchini Ujerumani,kiliuma katika kanda mbali mbali isipokua Afrika:
Kinyan’ganyiro hiki hivi punde kilizusha upya hofu za kuzuka fujo la mashabiki viwanjani wakati wa Kombe la dunia:Kwani fujo limetokea karibuni pale wenyeji wa Kombe lijalo la dunia-Ujerumani walipocheza dimba la kirafiki na Slovenia.
Mashabiki wakazusha fujo uwanjani mjini Bamako,Mali pale bao la dakika ya mwisho ya 90 la Togo,lilipoitoa Mali kabisa katika kinyan’ganyiro cha Kombe la dunia.Halafu mjini Pyongayang, wachezaji wa timu ya korea walizusha fujo uwanjani na kumuandama rifu wa kisyria na mwishoe kuihatarisha timu nzima ya Iran,baada ya kulazwa 2:1.
Hali hii mpya, imeongeza wasi wasi juu ya usalama viwanjani na sio tu huko Afrika na Asia, bali hata hapa Ujerumani-wenyeji wa Kombe lijalo la dunia.ilikuwa mashabiki wa Ujerumani waliozusha fujo wiki iliopita huko Slovenia ambako Ujerumani ilishinda chupuchupu tu kwa bao 1:0 .
Wakuu wa Ujerumani kwahivyo, wameahidi kuimarisha usalama kwa Kombe la dunia 2006 na wanadai hakutarejewa tena visa vya fujo lililoonekana katika mji wa Celje wa Slovenia,jumamosi iliopita.Huko wahuni 45 wa kijerumani walitiwa nguvuni kwa kuzusha fujo tangu mjini humo hata mikahawani na uwanjani.
Bw.Alfred Sengle,mkuu wa usalama wa Shirikisho la kabumbu la Ujerumani (DFB) ameungama hatahivyo, kwamba visa vya Slovenia vitailazimisha Ujerumani kudurusu upya utaratibu wao wa usalama kwa Kombe la dunia litakaloanza Juni 9 hadi finali Julai 9,mwakani.
Franz Beckenbauer, mwenyekiti wa Tume ya maandalio ya Kombe hilo la dunia ,alidai wiki hii kwamba waslovania walishindwa kuidhibiti hali ya mambo na akaahidi kwamba hatua za usalama Ujerumani zitakua kali mno.
Fujo la mashabiki wa Ujerumani jumamosi iliopita huko Slovenia, ni pigo jengine kwa Ujerumani ambayo karibuni tu dimba lake lilitiwadosari kwa kuibuka kashfa ya marifu waliopangilia matokeo kuvuna fedha katika vituo vya kamari.
Kwa sasa Ujerumani inajiwinda kuandaa Kombe la mashirikisho-CONFEDERATION CUP-linalofungua pazia la Kombe la dunia juni 15 mwaka huu hadi Juni 29.Ulimwengu mzima utakodoa macho kuona Ujerumani imejiandaa vipi na fujo za mashabiki na iwapo kweli itaweza kulinda usalama mwakani pale dunia nzima itakapokodoa macho Ujerumani kwa Kombe la dunia.
Katika uchunguzi uliofanywa ,imegunduliwa ni mashabiki wa timu inayofungwa ndio wanaozusha fujo.hii imeonekana mjini Bamako,Mali na kati ya wiki hii mjini Pyongayang,Korea ya kaskazini.
Uchunguzi uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Cardiff,huko Wales,Uingereza,umetupia macho wagonjwa waliowasilishwa katika idara ya matibabu ya dharura.Tarakimu za muda wa siku kadhaa pale Wales inapocheza dimba au Rugby na wakati hakuna mechi.
Katika kipindi cha miaka 7,Idara ya matibabu ya dharura ya hospitali hiyo imewasajili majeruhi 27,840.Siku inapochezwa mechi,wauguzi hutibu kiasi cha watu 30 na huu ni muongezeko wa 50% kutoka siku za kawaida bila ya mechi ambapo kesi za wagonjwa wanaotibiwa huwa 20 hivi.
Baada ya Korea ya kaskazini kuzabwa mabao 2:1 na Iran,fujo lilizuka uwanjani Pyongyang.Kocha wa Iran Branko Ivanovic alisema maisha ya wachezaji wake yalikua hatarini.
Sasa Japan ambayo ina miadi mwezi ujao ya kucheza pia Pyongyang mpambano wa Kombe la dunia,imeiingiwa na homa ya wasi wasi.wakati wa mpambano na Iran, wanajeshi wa Korea ya kaskazini waliitwa haraka kurejesha usalama miongoni mwa mashabiki 60.000 katika Kim Il-Sung stadium.Rifu na washika wake bendera hawakuweza kuondoka uwanjani kwa muda wa dakika 20 baada ya mchezo kumnalizika huku mashabiki waliokasirika wakivurumisha chupa,mawee na viti.
NJE YA FUJO LA DIMBA TIMU ZA KANDA MBALI MBALI ZILIKUA UWANJANI KATI YA WIKI KUNYAN’GANYIA TIKETI 31 KATI YA 32 ZA KOMBE LA DUNIA.
Ni Ujerumani tu kama mwenyeji ambayo haihitaji kuania nafasi.M;abingwa wa dunia Brazil wanabidi hata nao kukata tiketi yao.
Brazil ambao kamwe hawakuwahi kushinda nyumbani mwa Uruguay-Montevideo, walifaulu mara hii kutoka suluhu bao 1:1 na mabingwa wa kwanza kabisa wa dunia Uruguay.Diego Forland aliipatia Uruguay bao mapema kipindi cha pili kabla Emerson hakusawazisha kwa Brazil.Jogoo la Brazil Ronaldo lilishindwa tena kutamba katika mechi iliochezwa kwa kasi mbele ya mashabiki 60.000.Brazil kwa suluhu hiyo imepoteza pointi 2 ,lakini ipo bado nafasi ya pili nyuma ya viongozi wa kanda ya Amerika Kusini-Argentina.
Kocha wa Argentina Jose Pekerman aliipongeza timu yake baada ya kuvunja tumbuu ya lango la Colombia na kutia bao 1:0.Argentina ilitokwa na jasho kuvunja tumbu ya lango hilo,lakini mwishoe hodi-hodi zao ziiitikiwa-karibu.Argentina ilicheza nusu ya kipindi kizima na wachezaji 10 baada ya Fabian Vargas kutimuliwa nje ya chaki ya uwanja na rifu mnamo dakika ya 41 ya mchezo.
Sasa Argentina inaongoza kwa pointi 28 kanda hii ya timu 10,ikifuatwa na Brazil,Ecuador,Paraguay na Uruguay zinazodhibiti nafasi 5 za kwanza.Bolivia inaburura mkia wa kanda hii.
Brazil,ambayo haikuwahi kukosa kushiriki katika Kombe la dunia, itakutana na Argentina duru ijayo na baada ya kupoteza pointi 2 majuzi,haitamudu kupoteza pointi nyengine 3.
Katika kanda ya Ulaya,Holland iliokosa nafasi ya kushiriki Kombe lililopita la dunia, imechachama mara hii kutia na mapema mfukoni tiketi yake:
Holland iliizaba Armenia mabao 2:0 na mahasimu wao Jamhuri ya Czech katika kundi hili la kwanza,iliionea Andora kwa mabao 4:0.
Katika kundi la pili: Ukraine imeendelea kutamba na hadi sasa haikushindwa hata mara moja.Iliikomea Denmark bao 1:0-bao lililotiwa na Andriy Veronin anaeichezea Leverkusen katika Bundesliga.
Ama katika kundi la 3: Viongozi wa kundi hili-Ureno walitoka suluhu bao 1:1 na Slovakia yenye kusimama nafasi ya pili.
Maajabu yalizuka katika kundi la 4, kwani mabingwa wa dunia wa 1998 na wa Ulaya 2000-Ufaransa walizimwa na chipukizi Israel na kuondoka uwanjani sare bao 1:1. tangu Ufaransa hata Israel kila moja sasa ina pointi 10 kutoka mechi 6.Uswisi inafuata nyuma yao.
Wataliana wanaendelea kutamba katika kundi la 5: Tena hata kubidi jana kuingia uwanjani kwani ilitosha tu kwa mahasimu wao Moldova kutoka sare na Norway.
Katika kundi la 6: Uingereza,Poland na Austria zote ziliondoka jana na ushindi mbele ya Azerbaijan,ireland ya kaskazini na Belorusia.
England shukurani kwa mabao 2 ya Rooney,imesalia kileleni ikiwa na pointi 16.
Kundi la 7 si wazi kabisa kwani timu zote zimechachamaa:Serbia na Montenegro zimeizima Spain 0:0,Bosnia ikatoka suluhu 1:1 na Lithuania na Ubelgiji ilitokwa na jasho kabla kuizika San Marino kwa mabao 2-1.
Katika kumndi la 8 na la mwisho-kanda ya Ulaya: Croatia sasa imeparamia kuileleni ikichukua usuikani kutoka Sweden baada ya kuizaba malta 3:0.Sweden ambayo jana haikucheza ina pointi 12.
Kombe la dunia litatanguliwa Juni mwaka huu na Kombe la mashirikisho likijumuisha timu 8 hapa Ujerumani pamoja na mabimngwa wa dunia-Brazil na
wa Afrika Tunesia.Ujerumani kama mwenyeji na Ugiriki kama mabingwa wa Ulaya zinashiriki pia.
OLIMPIK 2012:
Mji wa Paris unapigiwa upatu uko mbele kabisa katika kinyan’ganyiro cha kuania m ji gani utaandaa michezo ya Olimpik 2012.Rais wa Halmashauri Kuu ya Olimpik Ulimwenguni-IOC- Juan Antonio Samaranch, alikanusha kati ya wiki hii kwamba kinyan’ganyiro hicho hakijamalizikia kwa miji 3 tu kuwa mbioni na mengine haina matumaini.Mji wa M adrid na Moscow pia bado ina matumaini.hatahivyo, kwa muujibu wa duru ziliopo karibu na Tume ya IOC miji ya Paris,London na New York iko mbele ya miji hiyo mengine.
MBIO ZA MAGARI MANAMA,BAHREIN:
Bingwa mara 5 wa mbio za magari ulimwenguni za Grand Prix,mjerumani Michael Schumacher ambae hakuanza vyema msimu huu wa 2005 ,ameahidi kwamba tarudi kutia fora.Anatumai motokaa yake mpya ya Ferrari,itakua ufungo wa ushindi wake mwengine wa 6 mwaka huu.
Kesho basi ataingia barabarani huko Manama,Bahrein.Hadi sasa msimu huu Schumacher amenyakua pointi 2 baada ya kuzuwilika kutokana na hali mbaya ya hewa mwanzoni mwa mwezi huu huko Australia na kupitwa kabisa na mahasimu wake katika mbio za M alaysia.
Na kwa taarifa hiyo basi ndio sina budi kuishia hapo kwa leo.