Friedrich Merz ni nani, Kansela mtarajiwa wa Ujerumani?
23 Februari 2025Friedrich Merz, mwenyekiti wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union (CDU), anatarajiwa kuwa Kansela ajaye wa Ujerumani kulingana na makadirio ya uchaguzi mkuu wa Ujerumani uliofanyika Februari 23.
Kambi yake ya muungano wa mrengo wa wastani wa kulia wa vyama vya CDU/CSU imekuwa ikiongoza kwa muda mrefu katika uchunguzi wa maoni ya umma, ikiwa na takriban asilimia 30 kwenye kura za maoni, na Merz alitambuliwa kama mpinzani mkuu wa Kansela aliyeko madarakani, Olaf Scholz wa chama cha mrengo wa wastani wa kushoto cha Social Democrats (SPD).
Ushindi wake katika uchaguzi huu wa mwishoni mwa wiki unakamilisha kurejea kwa kushangaza kwa Merz, ambaye alirejea Bundestag mnamo 2021 baada ya kukaa nje ya siasa kwa miaka 12.
Merz mwenye umri wa miaka 69, atakuwa kansela mzee zaidi tangu Konrad Adenauer, kansela wa kwanza wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, ambaye alichukua madaraka mwaka 1949 akiwa na umri wa miaka 73.
Scholz na Merz wote ni wabobezi wa sheria - lakini kufanana kwao kunaishia hapo. Mwanasiasa mrefu wa CDU ni mtu wa haiba ya kuvutia, awe akiingia chumbani au akipanda jukwaani. Anaonekana kuwa karibu na watu na hata mwenye ucheshi anapozungumza ana kwa ana, ingawa mara nyingine haachi taswira bora anapoinama kuzungumza na watu, jambo analofanya mara kwa mara.
Nje ya siasa na kuingia kwenye biashara
Wakati Angela Merkel alipooanda ngazi kuongoza kundi la wabunge wa CDU mnamo 2002 na kuingia ofisi ya kansela mwaka 2005, Merz, ambaye alikuwa na msimamo wa kihafidhina zaidi, alijiondoa na akabaki nje ya siasa kwa miaka mingi.
Akilinganishwa na Merkel, ambaye alionekana kama mwanasiasa mtulivu na mwenye mkakati wa tahadhari, Merz anaonekana kuwa mwanasiasa wa aina tofauti kabisa, akiwa tayari zaidi kuchukua hatari za kisiasa.
Alifanya hivyo hivi karibuni, katika mkutano wa mwisho wa chama mwishoni mwa Januari kabla ya uchaguzi huu, ambapo alizua dhoruba ya kisiasa alipojaribu kupitisha muswada mgumu wa uhamiaji bungeni kwa msaada wa chama cha mrengo mkali wa kulia, Alternative for Germany (AfD).
Hatua hii ilisababisha mshtuko kote nchini, huku waandamanaji wakilaani ushirikiano huo kama uvunjaji wa kihistoria wa mwiko wa baada ya vita wa kushirikiana na mrengo mkali wa kulia. Hata hivyo, Merz aliitetea hatua yake kama kamari iliyolenga kudhoofisha mafanikio ya AfD inayopinga uhamiaji.
Merz mara nyingi alionekana kama mpinzani wa Merkel mwanzoni mwa miaka ya 2000. Mnamo 2001, alijitokeza kuwania ukansela kwa uchaguzi wa shirikisho wa 2002. Hata hivyo, wakati huo, CDU ilimchagua mwanasiasa wa CSU kutoka Bavaria, Edmund Stoiber, ambaye aligombea dhidi ya Kansela wa Social Democrats, Gerhard Schröder—na kushindwa. Merz alijiondoa polepole kutoka kwenye ulingo wa siasa na kurejea katika kazi yake kama mwanasheria. Mnamo 2009, hakugombea tena kiti cha Bundestag.
Merz anatokea Sauerland—eneo lenye milima midogo magharibi mwa Ujerumani—na ni Mkatoliki pamoja na kuwa mwanasheria, kama baba yake kabla yake. Hadi leo, anaishi karibu na mahali alipozaliwa. Mnamo 1989, akiwa na umri wa miaka 33, alikua mbunge wa Bunge la Ulaya kwa tiketi ya CDU. Miaka mitano baadaye, alihamia Bundestag na haraka akajipatia sifa kama mzungumzaji mahiri. Kauli zake ndani ya kundi la wabunge wa chama zilikuwa na uzito mkubwa.
Baada ya kuondoka siasa, Merz aliingia katika sekta ya biashara, akihudumu katika kampuni za kimataifa za sheria na kuwa mjumbe wa bodi ya kampuni mbalimbali kati ya 2005 na 2021. Aidha, kati ya 2016 na 2020, aliongoza bodi ya usimamizi ya kampuni kubwa ya uwekezaji BlackRock nchini Ujerumani.
Lakini baada ya Merkel kutangaza kuondoka kwenye siasa mwaka 2021, Merz alirejea na polepole akapanda ngazi tena. CDU ilimchagua kuwa kiongozi wa chama mnamo 2022 katika jaribio lake la tatu. Alikuwa na sifa ya kuwa mwakilishi wa sera za kiuchumi za kiliberali ndani ya mrengo wa kihafidhina wa CDU.
Kauli zenye utata
Merz alipiga kura kupinga kulegezwa kwa sheria za utoaji mimba na dhidi ya uchunguzi wa kijenetiki kabla ya upandikizaji katika miaka ya 1990. Pia alikumbukwa vibaya kwa kupiga kura dhidi ya kuharamisha ubakaji wa ndoa mnamo 1997.
Daima aliunga mkono nishati ya nyuklia na alishinikiza sera za kiuchumi za kiliberali pamoja na kupunguza urasimu. Takriban miaka 25 iliyopita, alilalamikia athari za sera ya uhamiaji ya Ujerumani, akazungumzia "matatizo na wageni" na kusisitiza kuwa lazima kuwe na "utamaduni mkuu wa mwongozo" nchini Ujerumani.
Sasa anafufua baadhi ya masuala haya tena—lakini katika hali tofauti kabisa ya kisiasa na kijamii nchini Ujerumani. Katika kipindi cha majadiliano ya kisiasa cha "Markus Lanz" mnamo Januari 2023, alilalamikia ukosefu wa ujumuishaji nchini Ujerumani na kudai kuwa kuna "watu ambao kwa kweli hawana sababu ya kuwepo Ujerumani, ambao tumewavumilia hapa kwa muda mrefu, ambao hatuwarudishi, hatuwafukuzi, kisha tunashangaa kuwa kuna matukio ya kupindukia kama haya."
Aliongeza kuwa baadhi ya baba waliwazuia walimu, hasa walimu wa kike, kuwa na mamlaka yoyote juu ya watoto wao, ambao aliwafananisha na "pasha wadogo"—kauli iliyozusha utata mkubwa kwa mawazo yake ya kibaguzi. Hata hivyo, hakukuwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa uongozi wa juu wa CDU. Baada ya enzi ya Merkel, wanasiasa wengi waaminifu kwake waliondoka.
Tangu kiangazi kilichopita, Merz amejikuta akilazimika kusahihisha na kutetea baadhi ya kauli zake mwenyewe, hususan kuhusiana na uhamiaji na ushirikiano na AfD.
Chama Chenye mwelekeo wa kihafidhina zaidi
Kwenye jukwaa la Berlin, Merz anadai kuwa kundi la wabunge wa CDU limepata mwelekeo mpya katika maeneo muhimu. Pia amenazisha , kuusukuma mbele na kuukamilisha mchakato huu ndani ya CDU kupitia mpango mpya wa msingi, ambao "unaturejesha kwenye njia sahihi."
Merz sasa anawakilisha CDU ambayo imekuwa ya kihafidhina zaidi, ingawa misimamo yake binafsi haijabadilika sana katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Mwezi Novemba, kufuatia kuvunjika kwa serikali ya muungano wa Scholz iliyojumuisha SPD, Chama cha Kijani, na FDP, Merz alielezea muungano huo kama "historia."
"Muungano wa trafiki ya taa haujashindwa kwa sababu ya FDP pekee," alisema wakati huo, "bali kwa sababu hakukuwa na msingi wa pamoja wa kushirikiana kama serikali tangu mwanzo kabisa."
‘Mrengo wa kushoto umekwisha’
Lakini sasa, Merz na CDU/CSU wanaweza kukabiliwa na tatizo lilelile: Watashirikiana na nani kuunda serikali ya muungano?
Merz amekataa mara kadhaa uwezekano wa kushirikiana na chama cha mrengo mkali wa kulia, AfD, tangu mapema Januari. Hata hivyo, siku ya Jumamosi, saa chache tu kabla ya uchaguzi, alizidisha ukosoaji wake kwa vyama vikuu vingine vya siasa vya Ujerumani.
Akiwa Munich kwenye mkutano wa mwisho wa kampeni, katika hotuba kali na yenye msisitizo mkubwa, Merz alidai kuwa "mrengo wa kushoto umekwisha. Hakuna tena wingi wa mrengo wa kushoto, wala siasa za mrengo wa kushoto nchini Ujerumani."
Soma pia: Friedrich Merz
Pia alilaani maandamano yaliyofanyika Jumamosi dhidi ya itkadi kali za mrengo wa kulia, akisema kwamba endapo atashinda, atafanya siasa kwa ajili ya "Wajerumani wengi wanaofikiria kwa usahihi" na si kwa "watu wa kijani au wa mrengo wa kushoto waliopoteza mwelekeo ulimwenguni."
Si jambo la kushangaza kwamba viongozi wa chama cha Social Democratic Party (SPD) hawakufurahishwa.
"Friedrich Merz anazidisha mgawanyiko katika mrengo wa kati wa demokrasia ya nchi yetu katika hatua za mwisho za kampeni ya uchaguzi," aliandika kiongozi wa SPD, Lars Klingbeil, kwenye mtandao wa kijamii X (zamani Twitter).
"Hivi sivyo mtu anayetaka kuwa kansela wa kila mtu anavyoongea," Katibu Mkuu wa SPD, Matthias Miersch, aliliambia shirika la habari dpa. "Hivi ndivyo mtu kama Trump mdogo anavyoongea."
Kabla ya uchaguzi, SPD ilitarajiwa kuwa mshirika wa karibu zaidi wa CDU katika kuunda serikali mpya ya Ujerumani.