Friedrich Merz ni nani, Kansela mpya wa Ujerumani?
6 Mei 2025Friedrich Merz, mwenyekiti wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union (CDU), sasa ni Kansela rasmi wa Ujerumani, baada ya kushinda katika duru ya pili ya upigaji kura bungeni Jumanne hii. Ushindi huo ulipatikana saa chache baada ya kushindwa katika duru ya kwanza, hali iliyozua mshangao mkubwa kwenye ulingo wa siasa.
Katika kura ya pili iliyofanyika alasiri, Merz alipata kura 325 kati ya 630 katika Bunge la Shirikisho (Bundestag), akivuka idadi ya kura 316 zinazohitajika kwa wingi wa moja kwa moja. Ushindi huo ulihitimisha safari ndefu ya kurudi kwake katika siasa kuu, baada ya kukaa nje ya bunge kwa miaka 12 kabla ya kurejea 2021.
Merz mwenye umri wa miaka 69, anakuwa Kansela mzee zaidi kuwahi kuchaguliwa tangu Konrad Adenauer mwaka 1949. Tofauti na mtangulizi wake Olaf Scholz, Merz ni mwanasiasa mwenye haiba ya moja kwa moja, anayejulikana kwa msimamo mkali kuhusu masuala ya uhamiaji na sera za kiuchumi za kiliberali.
Katika historia yake, Merz alijiondoa kwenye siasa mwaka 2009 na kuingia katika sekta ya biashara, ambapo alihudumu katika bodi za kampuni mbalimbali, ikiwemo BlackRock nchini Ujerumani. Hata hivyo, alirejea kwenye siasa baada ya Angela Merkel kutangaza kuondoka, na akachaguliwa kuwa kiongozi wa CDU mnamo 2022.
Mwelekeo wa kihafidhina zaidi
Chini ya uongozi wake, CDU imekuwa na mwelekeo wa kihafidhina zaidi. Ameonekana mara kadhaa kushinikiza sheria kali kuhusu uhamiaji na kukosoa siasa za mrengo wa kushoto, akisisitiza haja ya kuwa na "utamaduni mkuu wa mwongozo" wa Kijerumani.
Soma pia: Merz ashindwa kuwa kansela duru ya kwanza ya kura bungeni
Kabla ya uchaguzi wa Februari 23, muungano wa CDU/CSU ulikuwa ukiongoza kwa kura za maoni kwa wastani wa asilimia 30. Ushindi wa Merz ulitarajiwa na hatimaye kuthibitishwa na wabunge katika kura ya pili, baada ya kushindwa kwa kura sita katika duru ya kwanza.
Miezi miwili kabla ya uchaguzi huo, serikali ya muungano wa Scholz—iliyojumuisha SPD, Chama cha Kijani, na FDP—ilivunjika, na kusababisha uchaguzi wa mapema. Hali hiyo iliufungua mlango kwa Merz kurejea kama nguvu mpya ya kihafidhina.
Ingawa Merz alijikuta kwenye mgogoro baada ya kujaribu kushirikiana bungeni na chama cha mrengo mkali wa kulia, AfD, katika suala la uhamiaji, alitetea hatua hiyo kuwa mkakati wa kudhoofisha umaarufu wa chama hicho chenye msimamo mkali. Hatua hiyo ilikosolewa vikali, lakini haikumzuia kuibuka mshindi.
Sasa akiwa Kansela, Merz anakabiliwa na changamoto ya kuongoza taifa lililogawanyika kisiasa na kijamii, huku akiapa kuleta uthabiti na dira mpya ya kihafidhina kwa taifa hilo lenye ushawishi mkubwa barani Ulaya.