Friedrich Merz akabiliwa na kura ya pili baada ya anguko
6 Mei 2025Kiongozi wa chama cha kihafidhina nchini Ujerumani, Friedrich Merz, ameshindwa kuchaguliwa kuwa Kansela katika duru ya kwanza ya upigaji kura bungeni, na hivyo kulazimika kujaribu tena katika duru ya pili iliyopangwa kufanyika baadaye Jumanne hii. Taarifa hii imethibitishwa na vyanzo kutoka ndani ya chama chake.
Katika kura ya kwanza ya Jumanne, Merz alipata kura 310 kati ya wabunge 630 wa Bunge la Shirikisho (Bundestag), akihitaji kura 316 ili kushinda kwa wingi wa moja kwa moja. Ni mara ya kwanza tangu Vita vya Pili vya Dunia kwa mgombea wa Ukansela kushindwa katika duru ya kwanza ya kura ya bunge.
Kushindwa huku kumemwaibisha Merz hadharani, hasa ikizingatiwa kuwa muungano anaouongoza—unaoundwa na CDU (Christian Democratic Union), CSU cha Bavaria, na SPD (Social Democratic Party)—unamiliki viti 328 bungeni, zaidi ya vinavyohitajika kwa ushindi.
Matokeo haya yametikisa siasa za Ujerumani na kuwaacha washirika wake wakihaha kutafuta hatua ya kuchukua. Kulingana na Sheria ya Msingi ya Ujerumani (Katiba), wabunge sasa wana hadi siku 14 kumchagua Kansela kwa wingi wa moja kwa moja bila kikomo cha idadi ya duru za kura.
Bunge lapitisha maamuzi kunusuru hali
Baada ya majadiliano na wataalamu wa sheria, vyama vinavyounda muungano mpya walikubaliana kuitisha duru ya pili ya kura saa 9:15 alasiri (kwa saa za Ulaya ya Kati), ikiwa ni juhudi za haraka kumaliza mkwamo huo wa kisiasa.
Soma pia: Vyama vya CDU/CSU na SPD vyatia saini makubaliano ya kuunda serikali ya pamoja
Kimsingi, wagombea wengine wanaruhusiwa kuwania nafasi hiyo, lakini muungano huo umesisitiza kuwa Merz atawania tena, japokuwa bado haijulikani kwa nini alikosa uungwaji mkono wa kutosha kwenye kura ya siri.
Kwa sasa, serikali ya Kansela anayeondoka, Olaf Scholz, ataendelea na majukumu hadi Kansela mpya atakapochaguliwa. Hali hii ya mkwamo imetokea miezi miwili na nusu tu baada ya muungano wa CDU/CSU kushinda uchaguzi wa Februari uliosababishwa na kuvunjika kwa serikali ya Scholz mnamo Novemba.
Baada ya wiki kadhaa za mazungumzo, vyama vya kihafidhina na SPD walikubaliana kuunda serikali ya pamoja, makubaliano ambayo yalitiwa saini rasmi mjini Berlin siku ya Jumatatu kabla ya zoezi la kumchagua Kansela Jumanne. Hata hivyo, mchakato huo sasa umevurugika.
Kushindwa kwa Merz kunahitimisha miaka ya juhudi na mapambano ya kisiasa dhidi ya utawala wa aliyekuwa Kansela Angela Merkel.
Ni pigo kubwa kwa mwanasiasa huyo ambaye alikuwa karibu kabisa na kilele cha uongozi wa Ujerumani, lakini sasa anakabiliwa na maswali kuhusu uimara wa uungwaji mkono wake.