Merz afanya ziara ya kwanza Ufaransa na Poland
7 Mei 2025Ziara hiyo ambayo tayari ilishapangwa inafanyika siku moja baada ya kiongozi huyo mpya kuchaguliwa na bunge kuushika wadhifa huo katika duru ya pili ya kura.
Ameshika wadhifa huo wakati Ulaya ikipambana kukubaliana kuhusu hakikisho la kiusalama kwa Ukraine ambalo ni sehemu ya makubaliano yoyote ya kusitisha vita na Urusi. Inapambana pia kupata maelewano na Marekani baada ya Rais Donald Trump kutangaza kiwango kikubwa cha ushuru.
Soma zaidi: Friedrich Merz aapishwa kuwa Kansela wa Ujerumani
Jijini Paris, Merz atazungumza na Rais Emmanuel Macron aliyekuwa kiongzi wa kwanza kumpongeza baada ya kushika wadhifa wa Ukansela. Itakumbukwa kuwa wakati wa kampeni mwezi Januari Kansela huyo mpya wa Ujerumani ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Christian Democratic Union CDU aliahidi kuwa angefanya juhudi za kurekebisha mahusiano na majirani muhimu ambao ni Ufaransa na Poland.
Ziara yake ya baadaye Jumatano nchini Poland inaakisi namna Warsaw inavyozidi kuwa muhimu kwenye siasa za Ulaya kutokana na jukumu kubwa iliyonayo katika kuiunga mkono Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Merz kukutana na Donald Tusk Warsaw
Kulingana na chanzo cha kuaminika, suala muhimu katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk litakuwa namna serikali ya Merz ilivyojipanga kuongeza bajeti ya ulinzi. Wanatarajiwa pia kulizungumzia suala la kuwa na sera kali ya uhamiaji ya Umoja wa Ulaya.
Wakati Friedrich Merz anafanya ziara kwenye nchi hizo mbili siku moja baada ya kuapishwa kwake, Urusi imesema haina sababu za msingi za kuboresha ushirikiano na Ujerumani chini ya Kansela mpya Friedrich Merz.
Katika taarifa ya serikali iliyotolewa mapema Jumatano, Msemaji wa Serikali ya Urusi Maria Zakharova amesema pia kuwa mipango yoyote ya Ujerumani ya kuipatia Kyiv makombora ya masafa marefu aina ya Taurus, hayawezi kuiokoa Ukraine.
Kwa upande wake Rais wa China, Xi Jinping amempongeza Merz kwa kuchaguliwa kuwa Kansela wa Ujerumani akisema nchi hizo mbili zinapaswa kuboresha ushirikiano wao na kuboresha utandawazi wa kiuchumi. Miongoni mwa pongezi nyingine kwa Merz ni kutoka kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, na serikali ya Marekani.