Merz achaguliwa Kansela wa Ujerumani baada ya sarakasi
6 Mei 2025Kiongozi wa chama cha kihafidhina nchini Ujerumani, Friedrich Merz, amechaguliwa kuwa Kansela mpya wa nchi hiyo Jumanne hii katika duru ya pili ya upigaji kura, baada ya kushindwa kwa mshangao katika duru ya kwanza mapema siku hiyo. Katika kura hiyo ya pili, Merz alipata kura 325 kati ya 630 katika Bunge la Shirikisho (Bundestag), akivuka kiwango cha kura 316 kinachohitajika kwa wingi wa moja kwa moja.
Kushindwa kwa mara ya kwanza kulisababisha fedheha kubwa kwa Merz, hasa ikizingatiwa kuwa muungano anaouongoza—unaojumuisha vyama vya CDU (Christian Democratic Union), chama ndugu CSU cha Bavaria, na SPD (Social Democratic Party)—unashikilia viti 328 bungeni. Hili lilizusha maswali kuhusu mshikamano ndani wa muungano huo, na kulazimisha mashauriano ya haraka ya kisiasa na kisheria.
Baada ya mchakato huo wa pili, Merz sasa anatarajiwa kuapishwa rasmi na Rais Frank-Walter Steinmeier katika Ikulu ya Bellevue mjini Berlin, na hivyo kuchukua nafasi ya Kansela anayeondoka, Olaf Scholz.
Hatua Mpya Katika Siasa za Ujerumani
Kabla ya ushindi huo wa pili, hali ya kisiasa nchini Ujerumani ilikuwa imeingia katika sintofahamu. Katiba ya Msingi ya Ujerumani inaruhusu hadi siku 14 kwa bunge kumchagua Kansela kwa wingi kamili, na hakukuwa na kikomo cha duru za upigaji kura. Baada ya majadiliano na wanasheria, muungano wa Merz uliitisha duru ya pili ya kura saa 9:15 alasiri kwa saa za Berlin.
Soma pia: Merz ashindwa kuwa kansela duru ya kwanza ya kura bungeni
Japokuwa wagombea wengine waliruhusiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro, vyama vya muungano vilisisitiza kuwa Merz angali mgombea wao pekee. Kilichosababisha kushindwa kwake katika duru ya kwanza bado hakijaelezwa wazi, ikizingatiwa kura hiyo ilikuwa ya siri.
Serikali ya Scholz itaendelea na shughuli hadi Merz atakapokabidhiwa rasmi madaraka. Uchaguzi wa Februari uliomweka Merz karibu na madaraka ulifuatia kuvunjika kwa serikali ya awali ya muungano wa Scholz mnamo Novemba, hali iliyochochea mazungumzo ya wiki kadhaa yaliyomalizika kwa makubaliano ya serikali mpya.
Makubaliano hayo yalitiwa saini Jumatatu mjini Berlin, yakitarajiwa kufuatwa na uapisho wa Merz Jumanne. Hata hivyo, ushindi wa Merz ulizuiwa ghafla katika duru ya kwanza, ukionyesha mivutano ya ndani ya muungano wake.
Kuchaguliwa kwa Friedrich Merz kama Kansela wa kumi wa Ujerumani tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia ni mafanikio ya kihistoria baada ya safari ndefu ya kisiasa iliyojumuisha migongano ya muda mrefu na uongozi wa Angela Merkel. Ushindi wake unakuja katika kipindi cha changamoto nyingi kwa siasa za Ujerumani na Ulaya kwa ujumla.