FIFA yakemea ubaguzi wa rangi dhidi ya wachezaji
18 Agosti 2025Infantino anatoa matamshi hayo siku moja baada ya Christopher Antwi- Adjei wa Schalke kusema alifanyiwa unyanyasaji wa ubaguzi wa rangi katika mchezo wao dhidi ya Lokomotive Leipzig. Alipigiwa miluzi na mashabiki muda wote wa mechi baada ya kuripoti tukio hilo kwa viongozi.
Kwenye kisa kingine, mchezaji mmoja wa Kaiserslautern alifanyiwa vitendo vya kibaguzi walipokuwa wakijiandaa na mchezo dhidi ya RSV Eintracht, kocha wa timu hiyo alisema, ingawa hakumtaja mchezaji aliyeathirika.
"Haikubaliki kwamba matukio haya yametokea katika mechi mbili za DFB-Pokal nchini Ujerumani," Infantino aliandika kwenye mtandao wa kijamii.
"Kandanda halina nafasi ya ubaguzi wa rangi au aina yoyote ya ubaguzi." Kila mtu kwenye FIFA, na jamii nzima ya mpira wa miguu inasimama kidete na wale wote walioathiriwa na matukio haya." Polisi wa Ujerumani inachunguza madai hayo.
Na huko Uingereza, Mtu mmoja amekamatwa kwa tuhuma za ubaguzi wa rangi baada ya kumtusi mshambuliaji wa Bournemouth Antoine Semenyo wakati wa mchezo wa Ligi ya Premier huko England. Mtu huyo aliyekamatwa ameachiliwa kwa dhamana, polisi wamesema Jumatatu.
Polisi wa Merseyside walisema mtu huyo, 47 kutoka Liverpool hataruhusiwa kuingia kwenye mechi yoyote ya soka nchini Uingereza au kukaribia umbali wa maili moja (kilomita 1.6) ya uwanja wa soka nchini Uingereza.
Mwanamume huyo alikamatwa kwa tuhuma za ubaguzi wa rangi dhidi ya Semenyo, ambaye ni mchezaji mweusi, aliyeripoti kwa mwamuzi kwamba alinyanyaswa na mtazamaji katika nusu ya kwanza ya Mechi ya Bournemouth dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield siku ya Ijumaa.