FAO, WFP, UNICEF wataka msaada kuingia kwa wingi Gaza
29 Julai 2025Taarifa ya mashirika hayo imeeleza Jumanne kuwa msaada wa chakula unahitajika Gaza kwa wingi, mara moja na bila kizuizi chochote. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, Cindy McCain katika taarifa hiyo ya pamoja na Shirika la Chakula Duniani, FAO, na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto, UNICEF.
WFP: Ni muda wa kuchukua hatua
Kwa mujibu wa McCain misaada inapaswa kuendelea kuingia kila siku katika Ukanda wa Gaza, ili kuzuia baa la njaa. Ross Smith, Mkurugenzi wa Dharura wa WFP, amesema ni wazi maafa yanatokea mbele ya macho yao, na wanapongeza hatua ya kusitisha mapigano kwa muda ili kuruhusu kupelekwa misaada ya kiutu Gaza.
''Hali hii inatukumbusha majanga ya zamani nchini Ethiopia au Biafra katika karne iliyopita. Na ni wazi tunahitaji kuchukua hatua za haraka, hivyo hii sio tahadhari, bali wito wa kuchukua hatua,'' alifafanua Smith.
Aidha, Sofia Calltorp Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Wanawake mjini Geneva, anasema wanawake na wasichana wa Gaza wanakabiliwa na chaguo gumu la kubaki ndani na kufa njaa katika makaazi yao au kujitosa kutafuta chakula na maji katikati ya hatari kubwa ya kuuawa.
Katika hatua nyingine, kundi la Hamas limesema wajumbe wake wa usuluhishi wameondoka Doha, Qatar kuelekea Uturuki, kujadiliana yaliyojitokeza katika mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yaliyokwama.
Vyanzo vya Hamas vimeliambia Shirika la Habari la Ufaransa, AFP kwamba ujumbe wa ngazi ya juu wa kundi hilo unaongozwa na Mohammed Darwish Rais wa Baraza la Uongozi la Hamas, pamoja na mkuu wa usuluhishi, Khalil al-Hayya.
Ujumbe huo utafanya mikutano kadhaa na maafisa wa Uturuki kuhusu yaliyojiri katika mazungumzo ya Doha yaliyokwama wiki iliyopita. Kwa wiki mbili, wapatanishi waliokuwepo nchini Qatar walikuwa wakipambana kujaribu kupata muafaka ili kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas.
Soma zaidi: Mazungumzo ya amani Gaza yatatitwa na msimamo wa Israel
Wiki iliyopita, Marekani iliungana na Israel kuwaondoa wapatanishi wake katika majadiliano hayo, huku mjumbe wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, akilishutumu kundi la Hamas kwa kushindwa kufikia makubaliano na kusema kuwa nchi hiyo itafikiria kuchukua njia mbadala.
Wakati huo huo, duru za Kipalestina zimeeleza Jumanne kuwa wanajeshi wa Israel wamewaua watu 13 katika na kituo cha misaada ya kiutu katika Ukanda wa Gaza. Aidha, Wapalestina wengine 105 wamejeruhiwa katika tukio karibu na njia ya Netzarim, katikati ya ukanda huo. Njia ya Netzarim inaendeshwa na shirika la misaada linaloungwa mkono na Marekani na Israel la GHF.
(AFP, DPA, AP, Reuters)