Familia ya kiongozi wa LRA Joseph Kony yarejea Uganda
26 Februari 2025Kurudi kwao nchini kumelezwa na wawakilishi wa serikali za Uganda kuwa kielelezo cha mwendelezo wa kusambaratika kwa kundi hilo licha ya yeye kukataa kujisalimisha ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake kwa mujibu wa mashtaka yanayotarajiwa kuanza kusikilizwa mwezi septemba mwaka huu.
Familia hiyo ya Kony imewasili majira ya saa saba kwenye uwanja wa ndege wa Entebbe wakisindikizwa na afisa wa ngazi za juu wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati pamoja na mjumbe wa shirika la Pacis La Uholanzi. Judith Acan ambaye ni mke wa Kony pamoja na mabinti zake wawili na mvulana kwa jina Pope Kony wameonyesha furaha kurudi nchini. Akiwapokea rasmi kwa niaba ya serikali ya Uganda, waziri wa masuala ya Kaskazini mwa nchi Dkt Kenneth Omona ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati pamoja na ile ya Uholanzi kwa kuwezesha watu 157 waliokuwa waasi wa LRA kurudi nchini katika kipindi cha miaka mitano hivi. Amewathibitishia wanahabari kwamba familia hii ni ya kiongozi wa waasi wa LRAambao kwa hiari yao wameamua kurudi Uganda baada ya kukubali fursa waliyopewa.
Waziri Omona ameelezea kuwa kama ilivyo kwa wale wengine waliowatangulia, familia hii itasaidiwa kupitia mafunzo na nasaha maalum ili waweze kutangamana na jamii yao ya Acholi. Hivi karibuni Uganda ilipitia mpango kama huo kuwarudisha nyumbani raia 19 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati waliokuwa wamekuja wakiwa wake na watoto wa waasi wa LRA walioamua kuchukua fursa ya msamaha.
Hii ni baada ya wao kuelezea kuwa walipendelea kuishi na jamaa zao nchini mwao. Kulingana na afisa wa ngazi za juu wa serikali ya Afrika ya Kati Fulbert Gbangona - Dabir anayeshughulikia mpango wa kuwashughulikia wale wanaondokana na uasi na kutangamanishwa na jamii zao, Joseph Kony angali yuko katika mapori ya nchi hiyo lakini idadi kubwa ya waliokuwa waasi wameendelea kujiondoa kutoka kundi lake. Amefahamisha kuwa kwa sasa kundi la LRA si tishio tena kwa usalama wa nchi hiyo kwani hawaendeshi ukatili wowote dhidi ya raia.
Wawakilishi hao wawili wa serikali za Uganda na Afrika ya Kati wamehimiza waaasi wa LRA ambao wangali wana mashaka na kujisalimisha na kupata msahama wafanye hivyo. Mahakama ya kimataifa ICC hivi karibuni ilielezea kuwa itaanza kusikiliza kesi dhidi ya Joseph Kony hata kama hajakamatwa hadi sasa. Haijafahamika mara moja kutoka kwa jamaa zake hao kama ana nia ya kujisalimisha lakini wanasema yuko hai na anafahamu kila kinachondelea. Kundi la LRA lilisababisha maafa na mateso makubwa kaskazini mwa Uganda miaka ya tisini na walipofurushwa waliendelea na vitendo vyao katika mataifa ya Sudan Kusini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na katika taifa hilo la Afrika ya Kati.