EU yatishia kuirejeshea Iran vikwazo vya kimataifa
18 Julai 2025Wanadiplomasia wakuu wa Ulaya wamemweleza mwenzao wa Iran kuwa, wanadhamiria kurejesha vikwazovya Umoja wa Mataifa ikiwa Tehran haitapiga hatua katika makubaliano ya nyuklia.
Wanadiplomasia hao, kutoka Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Umoja wa Ulaya, walimwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi kuhusu azma yao ya kutumia utaratibu unaoruhusu kurejeshwa kwa vikwazo vyote vya kimataifa dhidi ya Iran ikiwa hakutowepo na maendeleo madhubuti kuelekea makubaliano ya mpango wa nyuklia wa Tehran kufikia mwishoni mwa majira ya joto.
Umoja wa Ulaya unatumia shinikizo ili kuishawishi Iran kuhusu udharura wa kurejea katika njia ya kidiplomasia bila kuchelewa, ili kufikia makubaliano thabiti na ya kudumu.
Kumekuwa na uvumi mwingi kuhusu mpango huo wa nyuklia tangu Israel na Marekani ziliposhambulia vituo vya kijeshi na nyuklia vya Iran mwezi Juni.