EU yatangaza msaada wa dola bil 1.8 kwa Mamlaka ya Palestina
15 Aprili 2025Umoja wa Ulaya umetangaza mpango wa msaada wa hadi euro bilioni 1.6 (sawa na dola bilioni 1.8) kwa ajili ya kusaidia Mamlaka ya Palestina na kugharamia miradi katika Ukingo wa Magharibi, Jerusalem, na Gaza inayokabiliwa na uharibifu mkubwa kutokana na mashambulizi ya Israel. Takriban euro milioni 576 zitatumika kufadhili miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali, huku euro milioni 82 zikitengwa kwa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Zaidi ya theluthi moja ya fedha hizo zitatolewa kama msaada wa moja kwa moja wa bajeti kwa Mamlaka ya Palestina, zikilenga kuimarisha utawala wa kidemokrasia, huduma za kijamii na maendeleo ya sekta binafsi. EU imesisitiza kuwa msaada huo utasaidia kuijengea Palestina msingi wa kuendesha utawala imara baada ya vita, hasa Gaza.
Soma pia:Idadi ya Wapalestina waliouawa Gaza yafikia 50,700
Kamishna wa EU wa eneo la Mediterania, Dubravka Šuica, amesema baada ya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Palestina Mohammad Mustafa kuwa Mamlaka ya Palestina yenye utendaji bora na mageuzi ya kiutawala, inapaswa kuwa mhimili wa utawala wa Gaza katika kipindi cha baada ya vita. Pia, sekta binafsi itapata hadi euro milioni 400 kama mikopo nafuu ili kuchochea uchumi wa ndani.