EU yatangaza duru mpya ya vikwazo dhidi ya Urusi
18 Julai 2025Nchi hizo 27 wanachama zinalenga kuiwekea shinikizo Ikulu ya Kremlin kwa kupunguza zaidi mapato ya Urusi yatoikanayo na usafirishaji wa mafuta kwa nchi zisizo wanachama wa Umoja wa Ulaya na hivyo kuiathiri sekta ya kifedha ya Urusi.
Duru hiyo ya 18 ya vikwazo vya kiuchumi kutoka Ulaya dhidi ya Urusi tangu uvamizi wake wa 2022 inajiri huku washirika wakitumai Rais wa Marekani Donald Trump atatimiza tishio lake la kuiadhibu Moscow kwa kukwamisha juhudi za amani. Akizungumza mjini Brussels, Waziri wa Ufaransa anayehusika na masuala ya Umoja wa Ulaya Benjamin Haddad amesema Ulaya itaendelea kuongeza shinikizo mpaka Urusi isitishe vita vyake. "Kwa hivyo, njia pekee ya kukomesha vita hivi, kurudisha pande zote kwenye meza ya mazungumzo na kuunda mazingira ya amani ya haki na ya kudumu barani Ulaya, ni kuongeza shinikizo kwa Urusi. Shinikizo la kijeshi kwa kuendelea kupeleka silaha kwa Ukraine, ambayo inajilinda kwa ujasiri, na kiuchumi kupitia vikwazo. Na duru hii ya 18 ya vikwazo ni hatua kubwa kwenda mbele."
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amesema vikwazo vilivyoidhinishwa leo ni vikali zaidi. Kallas amesema vinatuma ujumbe wa wazi kuwa Ulaya haitaacha kuiunga mkono Ukraine. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amepongeza kupitishwa kwa vikwazo hivyo akisema ni muhimu na vimekuja katika wakati mwafaka.
Slovakia yaondoa upinzani wake
Hatua hizo mpya ziliidhinishwa baada ya Slovakia kutupilia mbali kizuizi chake cha wiki nzima kufuatia mazungumzo na Umoja wa Ulaya kuhusu mipango tofauti ya kuondokana na uagizaji wa kutoka Urusi.
Kiongozi wa Slovakia ambaye ni mshirika wa Kremlin Robert Fico -- ambaye nchi yake inategemea nishati ya Urusi -- aliacha upinzani wake baada ya kupata kile alichokiita "dhamana" kutoka Brussels juu ya bei za baadaye za gesi.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot amesema vikwazo vya karibuni "havijawahi kushuhudiwa" na kusema kuwa ""pamoja na Marekani watamlazimisha (Rais wa Urusi) Vladimir Putin kusimamisha mapigano".
Kama sehemu ya vikwazo vipya, Umoja wa Ulaya umekubali kupunguza ukomo wake wa bei ya mafuta ya Urusi yanayouzwa nje kwa nchi zisizo wanachama au kuwa katika makubaliano yoyote ya kimataifa, hadi asilimia 15 chini ya thamani ya soko.
Ukomo wa bei uliowekwa na Kundi la G7 mwaka wa 2022 wa dola 60 kwa pipa, unalenga kupunguza kiwango cha pesa ambacho Urusi inapata kwa kusafirisha mafuta kwa nchi nyingine kote ulimwenguni kama vile China na India.
Chini ya mpango mpya wa Umoja wa Ulaya, unaotarajiwa kuungwa mkono na washirika wa G7 kama vile Uingereza na Canada, kiwango kipya kitaanzia dola 47.6 na kinaweza kurekebishwa kadri bei za mafuta zitakapobadilika katika siku za usoni.
Pia kuna hatua za kuzuia mabomba ya gesi ya Bahari ya Baltic ambayo yamefungwa ya Nord Stream 1 na 2 yasifunguliwe tena.
Duru ya hivi punde zaidi ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya inajiri baada ya Trump siku ya Jumatatu kutishia kuwawekea ushuru wanunuzi wa nishati ya Urusi ikiwa Urusi haitasitisha mapigano ndani ya siku 50.
Duru nyingi za vikwazo vya kimataifa zilizowekwa dhidi ya Moscow katika kipindi cha miaka mitatu na nusu tangu uvamizi wake zimeshindwa hadi sasa kudhoofisha uchumi wa Urusi au kupunguza harakati zake za vita.
afp