EU yapendekeza kusawazisha uhusiano wa kibiashara na China
24 Julai 2025Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ametoa wito wa "kusawazisha upya" uhusiano wa kibiashara kati ya Umoja huo EU na China. Wito huo ameutoa wakati wa mkutano wa kilele unaofanyika leo mjini Beijing huku Rais wa China Xi Jinping akisema uhusiano huo upo katika kile alichokiita "kipindi cha mabadiliko makubwa."
Matarajio yalikuwa madogo kuelekea kuanza kwa mkutano huo wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na China zinazoadhimisha miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati yao.
Hii ni kufuatia mvutano juu ya muundo wa mkutano huo wa Beijing ambao muda wake ulipunguzwa ghafla kutoka siku mbili hadi moja baada ya ombi la China.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa walikutana na Rais wa China Xi Jinping mwanzoni mwa mkutano huo ambao unatarajiwa kujadili masuala kadhaa kuanzia migogoro ya kibiashara duniani, usalama, vita vya Ukraine pamoja na mambo mengine.
Costa aihimiza China iishawishi Urusi kumaliza vita nchini Ukraine
Mkutano huo unafanyika wakati ulimwengu ukishuhudia mizozo katika eneo la Mashariki ya Kati na vita vya Ukraine pamoja na tishio la ushuru wa Marekani.
Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa ameihimiza China kutumia ushawishi wake kwa Urusi kuvimaliza vita vya Ukraine - ombi la mrefu kutoka kwa viongozi wa Ulaya ambalo huenda likafungiwa macho tena.
"Tunapaswa pia kutetea maadili ya msingi yaliyomo kwenye Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambao tunasherehekea miaka 80 tangu kuanzishwa kwake—maadili kama vile mamlaka ya taifa, umiliki wa ardhi, na heshima kwa mipaka inayotambulika kimataifa. Kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, tunaiomba China kutumia ushawishi wake kwa Urusi ili iheshimu Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kumaliza vita vyake nchini Ukraine."
Rais huyo wa Baraza la Ulaya ameeleza pia uwezekano wa kufikia makubaliano kuhusu mabadiliko ya tabianchi, na kuongeza kwamba anatarajia "ujumbe thabiti wa kisiasa na wa pamoja” kutoka kwenye mkutano huo kueleka kwa mazungumzo ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa utakaofanyika mwezi Novemba nchini Brazil.
Ujumbe huo unatarajiwa kutolewa baadaye hii leo baada ya mazungumzo yao na Waziri Mkuu wa China Li Qiang.
Kwa upande wake, Rais Xi wa China amehimiza ushirikiano zaidi kati ya China na Ulaya kama nyenzo ya kuleta uthabiti katika dunia inayozidi kukumbwa na changamoto.
"Kadri hali ya kimataifa inavyozidi kuwa ngumu, ndivyo China na Umoja wa Ulaya zinapaswa kuimarisha mawasiliano, kukuza uaminifu wa pande zote, na kuendeleza ushirikiano—ili kuchangia uthabiti na usalama duniani kupitia uhusiano imara na mzuri kati ya China na EU."
Xi amesema pande zote mbili - Beijing na Brussels zinapaswa kuweka kando tofauti zao na kushirikiana kwa ukaribu.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa China iko tayari kutoa mchango zaidi katika kushughulikia athari zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Pia amekosoa vikwazo vya kanda hiyo ya Umoja wa Ulaya dhidi ya bidhaa za China zinazouzwa nje ya nchi.