EU yamtaka Rais Salva Kiir autulize mvutano nchini mwake
28 Machi 2025Umoja wa Ulaya umeonyesha wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuzuiliwa nyumbani kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar. Msemaji wa tume ya Umoja wa Ulaya, Anouar El Anouni, amesema Umoja huo unatoa wito kwa Rais Salva Kiir abadili hatua yake ili kuituliza hali nchini mwake.
Wakati huohuo Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, imechukua hatua ya kupunguza uwepo wa wafanyakazi wake katika taifa hilo la Afrika Mashariki kutokana na kuzorota kwa usalama.
Kukamatwa kwa Machar kumeashiria kuongezeka kwa hali ya wasiwasi katika nchi hiyo changa zaidi duniani. Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu nchini Sudan Kusini Yasmin Sooka amesema: "Sudan Kusini imesimama katika njia panda lakini uongozi wake unaweza kuamua kuheshimu makubaliano ya amani na kuendeleza mafanikio ya miaka saba iliyopita ya makubaliano hayo. Lakini ikiwa wataamua kutofanya hivyo, basi bila shaka wanaipandikiza Sudan Kusini katika mzozo mwingine."
Makubaliano ya kugawana madaraka kati ya Kiir na Machar yamekuwa yakivurugika taratibu, na hivyo kuhatarisha nchi ya Sudan Kusini kurejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu wapatao 400,000 kati ya mwaka 2013 na 2018.
Soma pia: UN yaelezea hofu ya Sudan Kusini kurejea katika vita
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga amewasili mjini Juba. Rais wa Kenya William Ruto, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, amemtuma Sudan Kusini Raila Odinga kama hii leo Ijumaa kama mpatanishi katika mzozo unaozidi kuongezeka nchini Sudan Kusini, ambao unatishia kusambaratisha mkataba tete wa amani kati ya pande mbili zinazohasimiana.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake kuhusu matukio ya nchini Sudan Kusini, akisema kuwekwa kizuizini kwa makamu wa kwanza wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar, kunaisogeza nchi hiyo karibu na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka viongozi wa Sudan Kusini "kutatua matatizo yao" kwa kuzingatia na kuyaweka mbele maslahi ya wananchi wa Sudan Kusini.
Vyanzo: AFP/AP