EU yaidhinisha orodha nyingine ya vikwazo kwa Urusi
14 Mei 2025Umoja wa Ulaya leo Jumatano umeidhinisha orodha nyingine ya vikwazo dhidi ya Urusi na kuahidi kuendelea kuchukua hatua zaidi ikiwa Urusi haitoikubali usitishaji wa mapigano huko Ukraine.
Hatua hiyo mpya dhidi ya Kremlin ambayo ni duru ya 17 ya vikwazo kutoka kwa Umoja wa Ulaya tangu Urusi ilipovamia Ukraine mwaka 2022 ilikuwa tayari mbioni hata kabla ya Marekani kuanza juhudi zake za upatanishi kati ya Urusi na Ukraine.
Soma zaidi: Urusi yakataa kupangiwa na EU kusitisha vita Ukraine
Makumi ya maafisa wa Urusi wataongezwa katika orodha hiyo ambayo tayari inayo karibu watu 2,400 wanaokabiliwa na marufuku ya kusafiri na mali zao kuzuiwa.
Haya yanajiri huku kukiwa na uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya rais wa Urusi Vladimir Putin na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky nchini Uturuki siku ya Alhamisi.