EU kuweka shinikizo la kuondoa ushuru mpya wa Trump
7 Aprili 2025Hata hivyo ikihitajika wanajiandaa kuchukua hatua za kupambana na hali hiyo ili kuepusha vita vya kiuchumi kati ya Ulaya na Marekani.
Jumuiya hiyo ya mataifa 27 inakabiliana na kodi za hadi asilimia 25 kwenye bidhaa za chuma na alumini na magari kadhalika zile za kulipizana kisasi za asilimia 20 kwenye bidhaa nyengine.
Amri hiyo inaanza kufanya kazi kesho Jumatano chini ya sera mpya ya rais Donald Trump wa Marekani inayolenga kuzigonga nchi zinazotoza bidhaa zao kodi ya juu.
Soma pia:Mawaziri wa biashara wa EU kujadili hatua za kujibu ushuru wa Marekani
Mawaziri hao wa Ulaya wa biashara wanakutana mjini Luxembourg kujadili njia mwafaka za kupambana na sera hiyo mpya ya Marekani kadhalika uhusiano wake na China.
Inasadikika kuwa azma yao ni kurejea kwenye mazungumzo ya kufikia suluhu na wala sio vita vya kibiashara na Marekani.Kauli hizo zinaungwa mkono na waziri wa Uholanzi wa Biashara Reinette Klever aliyekuwako mjini Luxembourg.
"Kwanza kabisa nadhani ni muhimu tusikurupuke…..ndipo tuweze kuchukua hatua mujarab zinazoendana na hali halisi.Kwahiyo, mwanzo,tunataka tukae chini na waMarekani ili tuone jinsi ya kushusha kodi hizo. Hata hivyo, hatutasita kuwa tayari na mikakati ya kupambana na hali iwapo itahitajika kushinikiza Marekani kukaa nasi kwenye meza ya mazungumzo.”
Mazunguzo ya kupata muafaka yagonga mwamba
Duru zinaeleza kuwa mazungumzo na Marekani yamegonga mwamba kufikia sasa.Kwa mujibu wa kamishna wa Umoja wa Ulaya wa biashara Maros Sefcovic,kikao chake na mwenzake wa Marekani cha Ijumaa iliyopita kilikuwa cha uwazi na kwamba alielezea kodi hizo kuwa zinawaathiri na hazikuwa za haki.
Umoja wa Ulaya huenda ukaridhia wiki hii awamu ya kwanza ya kodi za hadi dola bilioni 28 kwa bidhaa inazoagiza kutoka Marekani kuanzia bidhaa za meno hadi almasi ili kulipiza kodi itakayotozwa bidhaa zake za chuma na alumini.
Hatua hiyo haijaishtua Marekani ambayo sasa inatishia pia kuvitoza vinywaji vya pombe vya Ulaya kodi ya hadi asilimi 200 iwapo pombe yake kali ya Bourbon itatozwa kodi ya hadi asilimia 50.
Soma pia:Mataifa 50 yasaka mazungumzo na kibiashara na Marekani kuhusu ushuru wa Trump
Ifahamike kuwa Ufaransa na Italia ndiyo wauzaji wakubwa wa mvinyo na pombe kali barani Ulaya na wametiwa shaka na sera ya Marekani.
Umoja wa Ulaya unatazamiwa kutangaza hatua mpya za kodi za kulipiza kisasi ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.
Baadhi ya nchi wanachama zimetoa tahadhari na kusisitiza kuwa umoja unawapa nguvu zaidi.Waziri wa Ujerumani wa Uchumi anayeondoka Robert Habeck alisisitiza kuwa Jumuiya ina sauti kubwa zaidi ikiungana kwenye suala hilo.