EU kuondoa vikwazo katika sekta ya benki na nishati Syria
21 Februari 2025Umoja wa Ulaya siku ya Jumatatu utasitisha vikwazo kwa sekta za benki, nishati na usafiri nchini Syria katika juhudi za kusaidia ujenzi wa nchi hiyo baada ya kuondolewa madarakani kwa Bashar al-Assad. Haya ni kulingana na wanadiplomasia.
Hatua hiyo inayotarajiwa kuidhinishwa katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, ni rasmi baada ya umoja huo kufikia makubaliano ya awali mwezi uliopita kuondoa vikwazo katika maeneo muhimu.
Wanadiplomasia waliozungumza leo, wamesema vikwazo hivyo vinaweza kurudishwa tena ikiwa viongozi wapya wa Syria watavunja ahadi ya kuheshimu haki za walio wachache na kuelekea kwenye demokrasia.Jumuiya ya kimataifa yaunga mkono mpito mpya wa Syria
Siku ya Alhamisi, Umoja wa Mataifa ulisema kwa viwango vya sasa vya ukuaji, Syria itahitaji zaidi ya miaka 50 kurejea katika kiwango chake cha kiuchumi cha kabla ya vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe .