EU inapanga kampeni ya shinikizo dhidi ya Israel kuhusu Gaza
11 Julai 2025Wanadiplomasia wamesema Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amezitumia nchi wanachama orodha ya hatua ambazo kinadharia zinaweza kutumika kuishinikiza serikali ya Israel. Hatua hizo ni pamoja na kusitisha faida za kibiashara, kuweka vikwazo vya silaha, na kuizuia Israel kufaidika na mpango wa Umoja wa Ulaya wa ufadhili wa utafiti unaojulikana kama Horizon.
Soma pia: EU na Israel zakubaliana kuboresha misaada kwa Wapalestina
Hatua hizo pia zinaweza kuhusisha uimarishaji wa masharti ya kuingia Ulaya kwa raia wa Israel na kuweka vikwazo kwa wanasiasa wanaoonekana kuhusika na janga la hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza. Makubaliano ya usafiri wa anga kati ya Umoja wa Ulaya na Israel, ambayo yalifungua soko la safari za moja kwa moja za ndege kati ya Israel na Umoja wa Ulaya, pia yalitajwa kama suala linaloweza kutumika kwenye vikwazo hivyo.
Duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano katika eneo la Ukanda wa Gaza imeendelea huko Qatar, ambapo hatua zimepigwa kuhusu baadhi ya masuala yaliyoleta mjadala mkubwa.