Ethiopia yazindua mradi mkubwa zaidi wa umeme wa maji Afrika
9 Septemba 2025Hata hivyo, uzinduzi wa mradi huo umeibua mvutano wa kidiplomasia na baadhi ya majirani wake.
Kwa Ethiopia, bwawa hilo la Grand Ethiopian Renaissance Dam, GERD, ni mradi wa kitaifa na wa kihistoria na unaonekana kama ishara adimu ya mshikamano katika nchi ambayo imekumbwa na migogoro ya ndani kwa muda mrefu.
Bwawa hilo linalosimama kwa urefu wa mita 145 na kuenea takriban kilomita mbili juu ya mto Nile karibu na mpaka wa Sudan, limegharimu takriban dola bilioni nne. Limeundwa kuhifadhi maji yenye ujazo wa bilioni 74 na kuzalisha megawati 5,000 za umeme – ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya uwezo wa sasa wa uzalishaji wa nishati nchini Ethiopia.
Hata hivyo, nchi jirani ya Misri inayotegemea pakubwa maji ya mto Nile, inauona mradi huo kama tishio kubwa kwake.
Rais Abdel Fattah al-Sisi ameendelea kusisitiza kwamba Misri itachukua hatua zote stahiki chini ya sheria za kimataifa ili kulinda usalama wake wa maji.