Ethiopia yazindua mradi mkubwa wa umeme Afrika
9 Septemba 2025Huu ni mradi wa kitaifa unaochukuliwa kama ishara ya mshikamano kwa taifa la Ethiopia, licha ya changamoto za kisiasa na migogoro ya ndani. Bwawa lina urefu wa mita 145 na lina uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 5,000 za umeme—zaidi ya mara mbili ya uwezo wa sasa wa nchi hiyo.
Katika hotuba yake ya uzinduzi, Waziri Mkuu Abiy Ahmed alisema bwawa hili ni ushindi kwa Ethiopia na kwa Waafrika wote, na akawataka watu wote weusi kuliona kama mfano wa mafanikio ya bara. Lakini si viongozi pekee wanaosherehekea. Raia wa kawaida pia wanaona matumaini mapya. Fanuse Adete, ni mama wa watoto saba.
"Awali maisha yetu ya kila siku yalitegemea taa za mafuta ya taa na mkaa, jambo lililotuletea changamoto kubwa. Tulibeba kuni kwenda sokoni, tukiuza ili kununua mafuta na mkate kwa watoto. Lakini sasa baada ya bwawa kukamilika, jamii yetu yote inafuraha."
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi ya asilimia 45 ya wananchi milioni 130 wa Ethiopia hawana umeme. Wachambuzi wanasema mradi huu unaweza kubadilisha uchumi wa nchi, kuongeza uzalishaji wa viwandani na kupeleka nishati hata kwa majirani kupitia gridi ya kikanda inayoweza kufika Tanzania, Rwanda na Kongo.
Bwawa GERD limezua mvutano mkali wa kidiplomasia kati ya nchi jirani
Habtamu itefa, ni waziri wa Maji wa Ethiopia amesema baada ya hatua hiyo kubwa kilichobakia ni kutafuta wawekezaji zaidi.
"Sasa kwenda mbele tushirikiane kuvutia uwekezaji zaidi. Tuungane kuanzisha miradi inayoweza kutunufaisha wote, iwe Uganda, Tanzania, Rwanda, DRC, Sudan Kusini, Kenya, Ethiopia na hata Misri. Huo ndio mwelekeo tunaopaswa kuutazama," alisema Habtamu itefa.
Lakini mvutano unabaki. Misri yenye watu milioni 110 inalitegemea Ziwa Nile kwa asilimia 97 ya mahitaji yake ya maji. Rais Abdel Fattah al-Sisi amelitaja bwawa hilo kuwa "tishio la kimsingi kwa uhai wa Misri” na ameapa kulinda haki za maji za taifa lake kwa gharama yoyote chini ya sheria za kimataifa.
Jitihada za upatanishi kutoka Marekani, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na hata mataifa ya Ghuba zimegonga mwamba kwa miaka zaidi ya kumi. Wachambuzi wanasema mvutano huu hauhusu maji pekee bali pia usalama wa kitaifa na uthabiti wa kisiasa katika ukanda wa Afrika Kaskazini na Pembe ya Afrika.
Kwa upande wa Ethiopia, Abiy Ahmed anaona bwawa hili kama ishara ya "kuruka kuelekea mustakabali”, akilitumia pia kama chombo cha mshikamano wa kitaifa wakati taifa lake likikabiliwa na changamoto nyingi za ndani.