Ethiopia yakipiga marufuku chama cha kihistoria cha upinzani
15 Mei 2025Nchi ya Ethiopia ikielekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao, chama cha upinzani cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) kinakumbwa na hali ngumu baada ya kupigwa marufuku kujihusisha na shughuli za kisiasa. Hatua hiyo imezidi kufifisha matumaini ya chama hicho kushika tena madaraka katika taifa hilo la Pembe ya Afrika.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Ethiopia, hatua hiyo inafuatia kushindwa kwa TPLF kufanya mkutano wake mkuu, licha ya onyo kali la kusimamishwa kwa miezi mitatu lililotolewa mwezi Februari mwaka huu.
Tume hiyo ililitaka chama hicho kuchukua hatua za haraka kurekebisha kasoro za ndani, ikiwemo uchaguzi wa viongozi, lakini TPLF ilikaa kimya.
TPLF, ambacho kiliongoza mapinduzi ya mwaka 1991 na kutawala siasa za Ethiopia kwa miongo kadhaa, kimejikuta kikisuasua kutokana na migogoro ya ndani na ukosefu wa umoja miongoni mwa wanachama wake.
Kutotimiza masharti ya usajili wa vyama kunamaanisha kuwa hakitaweza kushiriki katika shughuli za kisiasa—ikiwa ni pigo kubwa kwa juhudi zake za kurejea madarakani.
Soma pia: Abiy asema yuko tayari kuongoza mapambano dhidi ya TPLF
Wachambuzi wa kisiasa wanaonya kuwa uamuzi wa kukifuta chama hicho kutoka usajili unaweza kuzua mvutano mpya kati ya serikali ya shirikisho na jimbo la Tigray, ngome ya TPLF.
"Hatua hii inaweza kuisukuma TPLF kutafakari upya ushirikiano mpya na wahusika wengine wa kisiasa nchini Ethiopia na kanda," alisema Kjetil Tronvoll, mtaalamu wa masuala ya Pembe ya Afrika, alipoongea na shirika la habari la AFP.
TPLF itahitaji kuomba upya usajili ili kushiriki uchaguzi
Chama hicho kilipoteza hadhi yake rasmi mwaka 2020 kufuatia kuanza kwa mzozo wa kivita kati ya majeshi yake na yale ya serikali ya shirikisho. Hata hivyo, baada ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa baadaye, TPLF kilirejeshwa kisheria kama chama cha kisiasa, hali ambayo sasa imebadilika tena.
Pamoja na hayo, TPLF bado kina fursa ya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Ethiopia unaotarajiwa kufanyika mwezi Juni 2026, iwapo kitaomba na kupatiwa usajili upya na kutimiza masharti yote yaliyowekwa.
Mwaka 2020, jimbo la Tigray lilikumbwa na mzozo mkubwa wa silaha kati ya TPLF na serikali ya shirikisho, mzozo uliodumu kwa miaka miwili na kusababisha vifo vya watu takriban 600,000, kwa mujibu wa makadirio ya taasisi za kimataifa.
Mustakabali wa TPLF sasa unasalia kuwa katika hali ya sintofahamu, huku wadau wa ndani na nje ya Ethiopia wakiangazia iwapo chama hicho kitarejea tena kama nguvu ya kisiasa au kubakia historia ya siasa za taifa hilo.