Eritrea yaionya Ethiopia dhidi ya kuanzisha vita vipya
21 Julai 2025Eritrea na Ethiopia zimekuwa na uhusiano mbaya tangu Eritrea kujitangazia uhuru wake mwaka 1993 na vita kati yao kuwaua maelfu katika kipindi cha mwaka 1998 hadi 2000.
Chanzo cha mzozo huo mpya kulingana na serikali ya Eritrea ni azma ya muda mrefu ya jirani Ethiopia kutumia eneo la bandari.
Rais Afwerki anayeiongoza Eritrea kwa mkono wa chuma tangu ijitangazia uhuru wake,amemtahadharisha mwenzake wa Ethiopia kuwa hawataweza kuwashinda nguvu kwasababu ya idadi yao pekee.
Ifahamike kuwa Ethiopia ina jumla ya wakaazi milioni 130 nayo Eritrea in watu milioni 3.5.
Akilihutubia taifa kupitia kituo rasmi cha televisheni,Rais Afwerki alisisitiza kuwa Ethiopia inajidanganya kwa kudhani kuwa idadi ya watu wake ni silaha dhidi yao.
Kiongozi huyo alishikilia kuwa Ethiopia inapaswa kutafutia suluhu matatizo yake ya ndani kabla ya kuwahusisha watu wake na vita visivyowahusu.
Alielezea kuwa vitendo vya Waziri Mkuu Abiy wa Ethiopia ni juhudi za kipuuzi za kujisogeza kando na matatizo yao ya ndani.
Fukuto la Mzozo halijasahaulika
Itakumbukwa kuwa Rais Abiy alitiliana saini mkataba wa amani na mwenzake Afwerki pindi baada ya kuingia madarakani mwaka 2018, ila vita vikali vilizuka katika jimbo la Ethiopia la Tigray kati ya mwaka 2020 na 2022, huku vikosi vya Eritrea vikiwaunga mkono waasi waliokuwa wakipambana na wanajeshi wa Ethiopia.
Takwimu za Umoja wa Afrika zinaashiria kuwa watu wasiopungua laki 6 waliuawa kwenye mapigano hayo.
Ijapokuwa makubaliano ya amani yalivimaliza vita hivyo,vikosi vya Eritrea bado vinaendelea kupiga doria jimboni Tigray na uhusiano kati ya majirani hao wawili umevurugika.
Mwezi uliopita,shirika la utafiti la Marekani,liliinyoshea kidole cha lawama Eritrea kwa kuimarisha jeshi lake na kuwavuruga majirani.
Kulingana na waziri wa mawasiliano wa Eritrea Yemane Ghebremeskel aliyeikosoa ripoti hiyo ya shirika lisilo la kiserikali la The Sentry,uhasama na mivutano hii mipya ya kikanda imesababishwa na Ethiopia.
Eritrea iliwekewa vikwazo vya silaha na Marekani vilivyoondolewa mwaka 2018 baada ya makubaliano ya amani kufikiwa.
Utafiti unaiweka Eritrea kwenye nafasi mbaya ukizingatia utimizaji wa haki kulingana na tathmini ya waandishi bila mipaka nao Umoja wa Mataifa umeiweka kwenye nafasi ya 175 kati ya 183 kwenye orodha ya mataifa yanayotimiza vigezo vya maendeleo ya binadamu ya mwaka 2022.