Erdogan azungumza kwa simu na Putin juu ya vita vya Ukraine
20 Agosti 2025Mazungumzo hayo ya simu kati ya Putin na Erdogan yameweka wazi nafasi ya Uturuki kama mpatanishi wa kikanda, hasa ikizingatiwa uhusiano wa karibu wa Ankara na pande zote zinazohusika katika mzozo huo.
Erdogan amesisitiza kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana bila ya kufanyika mazungumzo ya wazi na kwa ushirikiano wa kimataifa.
Uturuki ambayo ina uhusiano wa karibu na majirani zake wote wawili wa Bahari Nyeusi – Urusi na Ukraine, imeandaa duru tatu za mazungumzo ya amani kati ya Moscow na Kyiv tangu mwezi Mei.
Ankara mara kwa mara imesisitiza juu ya kulindwa kwa mipaka ya Ukraine huku ikionekana kuepuka kuunga mkono vikwazo vya mataifa ya Magharibi dhidi ya Urusi.
Taarifa hiyo ya Uturuki inajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kufanya mazungumzo na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na viongozi wa Ulaya mjini Washington mapema wiki hii, siku tatu tu baada ya mkutano wa Trump na Putin uliofanyika katika jimbo la Alaska.
Mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO Mark Rutte pia alizungumza kwa njia ya simu na Erdogan siku ya Jumanne alipokuwa akirudi Ulaya baada ya mkutano huo wa Washington.
Ofisi ya Rais wa Uturuki imeeleza kwamba wawili hao - Rutte na Erdogan,walijadiliana kuhusu mchango wa Uturuki katika mchakato wa amani nchini Ukraine, kama moja ya nchi muhimu ndani ya jumuiya ya NATO.
Viongozi hao wawili pia walibadilishana mawazo kuhusu dhamana za usalama endelevu bila ya kutoa maelezo zaidi, taarifa hiyo ya Ikulu ya Rais wa Uturuki ilisema.
Urusi yatoa onyo kali juu ya kutoshirikishwa
Wakati mazungumzo ya kimataifa kuhusu dhamana za kiusalama kwa Ukraine yakiendelea, Urusi imetoa onyo kali kwa mataifa ya Magharibi, ikisema kuwa juhudi za kulitafutia ufumbuzi suala la usalama nchini Ukraine bila ya ushiriki wa Moscow ni sawa na "barabara isiyokuwa na mwisho."
Kauli hii imetolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ambaye amewakosoa vikali viongozi wa Ulaya waliokutana na Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White siku ya Jumatatu.
"Hatuwezi kukubaliana na pendekezo la kutatua masuala ya usalama wa pamoja bila ya kuishirikisha Urusi. Hili halitafanikiwa. Tayari tumeweka wazi mara kadhaa kwamba Urusi haizidishi masharti yake, lakini tutalinda maslahi yetu halali kwa uthabiti na ukali. Na nina hakika kwamba katika nchi za Magharibi, hasa Marekani, wanaelewa vyema kabisa kuwa kujadili kwa dhati masuala ya usalama bila Urusi ni ndoto tu—ni barabara isiyokuwa na mwisho."
Lavrov amesisitiza kuwa mazungumzo yoyote yanayolenga kuvimaliza vita vya Ukraine, ambavyo vimeendelea kwa zaidi ya miaka mitatu, hayawezi kufanikishwa bila ya kuishirikisha Urusi moja kwa moja. Mwanadiplomasia huyo aliongeza kuwa dhamana za kiusalama zinazojadiliwa kwa Ukraine zinaweza kuchochea mvutano zaidi ikiwa zitapitishwa bila ya makubaliano ya pande zote husika.
Lavrov badala yake amesema Urusi inaunga mkono "dhamana za kweli" kwa Ukraine, akieleza kuwa msingi wa dhamana hizo unaweza kuigwa kutoka katika rasimu ya makubaliano yaliyokuwa yakijadiliwa mjini Istanbul mwaka 2022, katika wiki za mwanzo za vita vya Ukraine.
Hata hivyo, Kyiv ilikataa pendekezo hilo la mwaka 2022 kwa sababu masharti ya Urusi yangetoa mamlaka ya turufu kwa Moscow juu ya mwitikio wowote wa kijeshi kutoka kwa washirika wa Ukraine, kumaanisha kwamba Urusi ingeweza kuzuia msaada wa kijeshi kwa Ukraine ikiwa isingekubaliana na hatua hiyo.