Erdogan asema hatosalimu amri kwa vitisho vya ghasia Uturuki
21 Machi 2025Hali hii inatokea katika wakati maandamano ya kupinga kukamatwa kwa meya wa mji wa Istanbul yanazidi kuwa makubwa.
Kiongozi huyo ameyasema hayo kupitia hotuba aliyoitoa leo siku moja baada ya kutokea makabiliano makali kwenye miji kadhaa ya Uturuki baina ya vikosi vya usalama na waandamanaji wanaolaani kuwekwa kizuizini kwa Meya wa Istanbul, Ekrem Imamoglu, anayezingatiwa pia kuwa mpinzani mkuu wa Rais Erdogan.
Soma pia: Wanamgambo wa kikurdi wa PKK watangaza usitishwaji mapigano
Imamoglu ambaye chama chake kinajiandaa kumtangaza kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2028, alikamatwa katikati ya wiki hii kwa madai ya rushwa na ugaidi na tangu wakati huo amebakia chini ya kizuizi cha polisi.
Viongozi wa miji mikubwa ikiwemo Istanbul, mji mkuu Ankara na jimbo la Izmir wametangaza kupiga marufuku ya mikusanyiko ya watu katika jitihada za kuzuia wimbi la maandamano ya umma.