Erdogan akutana na Rais Subianto wa Indonesia
12 Februari 2025Marais hao wawili wamekutana kwa ajili ya mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na ulinzi baina ya mataifa hayo yenye idadi kubwa ya waumini wa dini ya Kiislamu.
Mataifa hayo mawili yanafanya mkutano wao wa kwanza wa kilele wa Ngazi za Juu wa Baraza la Ushirikiano wa Kimkakati, baada ya kukubaliana kuunda jukwaa katika mkutano uliofanyika mjini Bali, mwaka 2022.
Indonesia ni taifa la pili kutembelewa na Erdogan katika ziara yake ya kikazi barani Asia. Mataifa mengine atakayoyatembelea ni Malaysia na Pakistan.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia Rolliansyah Soemirat alisema kwenye mkutano huo ni wa ngazi za juu zaidi, masuala yote muhimu ya maslahi ya pamoja yatajadiliwa, ikiwa ni pamoja na masuala ya kimkakati na vipaumbele.
Lakini taarifa ya serikali ya Uturuki ilisema mazungumzo yataangazia hali ya sasa ya kikanda na masuala ya kiulimwengu na hasa vita vya Gaza.